Mashirika ya Marekani, Uswis kuinufaisha Tanzania mradi wa saratani

Taasisi ya saratani ya Ocean road

Muktasari:

Takwimu zina onyesha kuwa wagonjwa wa saratani walioripoti katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI) waliongezeka  kutoka 4,195 mwaka 2014 na mwaka 2015 walifikia  5529.

Dar es Salaam. Tanzania ni kati ya nchi tatu za ukanda wa Afrika Mashariki zitakazonufaika katika mradi wa kupambana na saratani uliotangazwa na mashirika matatu ya kimataifa kutoka nchini Marekani na Uswiss.

Chama cha wataalamu wa uchunguzi wa magonjwa kutoka Marekani (ASCP) na chama cha wataalamu wa saratani kutoka Marekani(ACS) wamesema  watatekeleza mpango wa pamoja wa kuboresha matibabu ya saratani katika nchi za Uganda, Ethiopia na Tanzania.

 Kuna ongezeko  la wagonjwa wa saratani nchini. Takwimu zina onyesha kuwa wagonjwa wa saratani walioripoti katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI) waliongezeka kutoka 3776 mwaka 2013 hadi 4,195 mwaka 2014 na mwaka 2015 walifikia  5529.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa Ijumaa Novemba 17, chama cha ASCP  kimesema kitazijengea uwezo wa kufanya vipimo vya kimaabara nchi za Tanzania na Ethiopia, ikiawamo kuanzisha mtambo wa kikemia unaoweza kubaini tishu zenye saratani katika mwili wa binadamu.

 “Utaalamu huu ni muhimu kwa madaktari bingwa wa saratani katika  kubaini na kutibu magonwa mengi,’’ alisema Mwenyekiti  Mtendaji wa ASCO,  Blair Holladay.

 Nacho chama cha ACS, kilisema  kitatoa mafunzo kwa wataalamu wa saratani katika nchi ya Tanzania, Uganda na Ethiopia katika kuboresha miundo mbinu ya usafirishaji wa sampuli na utoaji wa dawa za kutibu saratani(Chemothreapy).

Kampuni ya kimataifa, Norvatis, kutoka nchini Uswis itatoa ufadhili wa kifedha ili kufanikisha miradi hiyo.

ACS wao walisema  tayari wameanza kufanya kazi na watalaamu katuka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika kubuni na kuboresha miongozo itakayo saidia katika kutibu Saratani nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Katika siku zijazo, ACS walisema , watajikita katika kuimarisha utabiri wa upungufu wa dawa za saratani nchini Tanzania ili kuweza kukabiliana na changamoto za manunuzi ya dawa hizo.

Mkuu wa kampuni ya Norvatis, Harald Nusser amesema mradi wa matibabu ya saratani utajikita katika kusaidia kutatua matatizo ambayo yakitatuliwa, yataleta matokeo chanya katika mapambano dhidi ya saratani.

“Dawa ni muhimu lakini pia kuejnga mifumo ya kimatibabu ni muhimu zaidi,’’ amesema  Nusser katika taarifa  kwa vyombo vya habari ambayo Mwananchi imepokea.

Ugonjwa wa saratani unazidi kukua barani Africa, hususani chini ya jangwa la Sahara. Takribani watu 650,000 hupatikana na saratani kila mwaka na vifo zaidi ya 510,000 hutokea kwasababu ya kukosa matibabu ya ugonjwa huo.