Mradi wa majitaka kuhamisha 169

Muktasari:

Katika mwaka huu wa fedha kupitia Mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WSP).

Dodoma. Wakazi 196 wa Nzuguni watahamishwa kwenye makazi yao ili kupisha mradi wa mabwawa ya majitaka yatakayojengwa kwenye eneo hilo.

Katika mwaka huu wa fedha kupitia Mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WSP).

Hatua hiyo ni miongoni mwa mipango ya Serikali kuhakikisha kuwa wakazi waliopo na watakaohamia wanapata huduma hiyo.

Akizungumza jana Meneja wa Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) Mhandisi Kashilimu Mayunga alisema Serikali imeshalipa fidia ya Sh611 milioni kwa wakazi wote 196 wanaotakiwa kuhama kwenye eneo hilo.

Alisema eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 60 linatarajiwa kujengwa mabwawa 10 yatakayotosheleza mahitaji ya wakazi wa Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Mhandisi David Palangyo alisema hivi sasa mabwawa yanayotumika yaliyopo eneo la Swaswa yameelemewa na hayatoshelezi mahitaji ya mji.

“Mabwawa ya majitaka yaliyopo eneo la Swasa yameelemewa lakini tumetenga maeneo kwa ajili ya kujenga mabwawa mapya ili kumaliza changamoto hii,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Duwasa, Sebastian Warioba alisema tayari Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) wameshapima eneo la kujenga mabwawa ya majitaka na kinachosubiriwa ni kuanza kwa mradi huo.

Alisema mradi huo utaanza katika mwaka huu wa fedha 2016/17 kwa kutumia fedha za mradi wa maji unaofadhiwa na Benki ya Dunia WSP2 awamu ya pili.

Alisema wakazi wa Dodoma wote wataweza kuhudumiwa katika mfumo wa majitakautakaoratibiwa na mamlaka hiyo.

Kwa upande wa majisafi, Mhandisi Palangyo alisema mahitaji ya huduma ya majisafi ni lita za ujazo 46,000 lakini wanao mtandao unaoweza kusambaza lita za ujazo 40,000 kwa siku.