Mradi wa nyumba 400 wampa Shein ‘jeuri’

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein

Muktasari:

Waziri aeleza ulivyoweza kutoa ajira 400 kwa wananchi

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema utekelezaji miradi si jambo la kukurupa bali ni mipango imara iliyoasisiwa chini ya uongozi wa CCM.

Alitoa kauli hiyo juzi akikabidhi nyumba 60 kwa wanunuzi katika mradi wa nyumba za unaoendeshwa na Fumba Development. Dk Shein alisema Serikali hupanga mipango yake kwa mujibu wa taratibu zake wala hailazimishwi kufanya miradi hovyo hovyo, ambayo ikitekelezwa inaweza kuharibu malengo yaliotarajiwa hasa suala la uwekezaji.

Alisema kutokana na Serikali kukabiliwa na uhaba wa fedha, ndiyo maana wamefungua milango kwa wawekezaji kuwekeza kwa mujibu wa taratibu na sheria ziliopo. Rais huyo alisema Serikali itafanya maboresho ya miundombinu ya barabara, maji, umeme na huduma ya ijamii ili kuwavutia zaidi wawekezaji.

Kuhusu ujenzi huo, alisema ukikamilika kitakuwa kichocheo kikubwa cha nchi kuimarika kiuchumi.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed alisema kuja kwa fursa za uwekezaji ni moja ya hatua kubwa za kuisaidia Serikali katika kuhudumia wananchi.

Dk Khalid alitolea mfano wa mradi huo kuwa hivi Sasa una zaidi ya wafanyakazi 400 ambao wananufaika kwa kufanya kazi mbalimbali.

Awali, mmiliki wa mradi huo, Sebastian Dietzold aliahidi kushirikiana na Serikali katika kuona mradi huo unawanufaisha wananchi, wawekezaji na Serikali.

Mradi huo ambao awamu ya kwanza utakuwa na nyumba 400, umegharimu zaidi ya Dola 280 milion za Marekani.