Mradi wa umeme wa Stiegler sasa rasmi

Dodoma. Serikali imeonyesha dhamira yake ya dhati ya kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme baada ya kutenga Sh700 bilioni kwa ajili ya mradi wa Stiegler’s Gorge, kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Nishati iliyowasilishwa bungeni jana.

Mradi huo, uliopewa jina la mgunduzi wa Uswisi aliyefia eneo hilo mwaka 1907 baada ya kushambuliwa na tembo, utajengwa katika Mto Rufiji, ndani ya Hifadhi ya Selous na unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,100 za umeme.

Akiwasilisha bajeti hiyo jana, Waziri wa Nishati, Dk Medrad Kalemani aliomba chombo hicho cha kutunga sheria kiidhinishe Sh1.69 trilioni kwa mwaka 2018/19, huku zaidi ya asilimia 40 zikitengwa kwa mradi huo unaotarajiwa kuanza Julai.

Dk Kalemani alisema mkandarasi atafanya kazi za awali kwa miezi mitatu kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36.

“Fedha za maendeleo za ndani Sh700 bilioni zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi hizo,” alisema.

Alizitaja kazi hizo kuwa ni ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi na njia kuu za kupitisha maji.

Dk Kalemani alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, kazi iliyofanyika ni uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na makandarasi walioonyesha nia ya kutekeleza mradi huo.

“Ujenzi wa njia ya msongo wa KV 33 kutoka Dakawa kwa ajili ya kupeleka umeme utakaotumiwa na mkandarasi wakati wa ujenzi wa mradi ulianza Novemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu,” alisema.

Mradi huo unatarajiwa kujengwa kwenye eneo la kilomita 1,350 za mraba na litajengwa bwawa lenye urefu wa mita 134.

Kwa mujibu wa mpango mkuu wa mfumo wa nishati wa mwaka 2016, mahitaji ya umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli za biashara yataongezeka hadi asilimia 18 kati ya mwaka 2015 na 2020 kutokana na maendeleo ya gesi, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, kuongezeka kwa uwekezaji kutoka nje, kukua kwa kiwango cha elimu na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano.

Katika mpango huo wa mwaka 2016, haja ya kuongeza uzalishaji umeme inaonekana kubwa kutokana na matumizi ya mkaa kufikia asilimia 80 na hivyo mikakati ya umeme kutarajiwa kupunguza matumizi hadi asilimia 49 ifikapo mwaka 2040.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamekuwa wakipinga kuanza kutekelezwa kwa mradi huo wakitaka kwanza ufanyike upembuzi yakinifu wa athari za kimazingira kabla ya utekelezaji kuanza, jambo ambalo Serikali imesema linafanyika na sasa timu yake imeenda eneo hilo kuzungumza na wadau.

Pia wanaharakati za mazingira wanadai kuwa utekelezaji wa mradi huo utaondoa hali ya uasilia wa eneo hilo na kusababisha viumbe, mimea na wananchi kuhamishwa kupisha mradi pamoja na kuathiri shughuli nyingine za kiuchumi kama utalii.

Lakini jana, Dk Kalemani alieleza umuhimu wa mradi huo mkubwa wa kuzalisha umeme akisema miongozi manufaa ya Stiegler’s Gorge ni kuvutia watalii, hivyo kuongeza fedha za kigeni, kuongezeka kwa shughuli za majini kama vile michezo ya majini.

Alisema visima 10 ndani ya bwawa vitaongeza mazalia ya samaki, mamba na viboko, hivyo kuvutia watalii.

Waziri alisema litajengwa tuta la kuzuia maji lenye urefu wa sawa na ghorofa 45 kwenda juu na upana wa kilomita moja litakalovutia utalii na hata kutumiwa na maharusi walio fungate.

Alisema manufaa mengine ni pamoja na kutunza maji katika bwawa la mradi yanayoweza kumwagilia hekta 250,000 za mashamba, hivyo kukuza shughuli za umwagiliaji. Alisema bwawa hilo litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 914.

Pia, kutoa huduma za kijamii katika maeneo ambayo yanazunguka mradi huo ikiwamo wananchi hao kuruhusiwa kufanya uvuvi.

Dk Kalemani alisema umeme utasambazwa maeneo ya vijiji 49 vya jirani kutoka wilaya za Morogoro Vijijini, Kibiti, Rufiji, Ulanga, Malinyi na Mlimba.

Alisema wananchi hawataondolewa wala kuhamishwa katika makazi yao na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasa) imeshaanza kufanya utafiti wa mahali watakapochukua maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani kwa wananchi wa Pwani na Dar es Salaam.

Katika mikoa hiyo, alisema maji yatapita katika vijiji vya wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Temeke na Kigamboni, hivyo kuingia katika mfumo wa maji wa Jiji la Dar es Salaam na kutoa ajira kwa watu 10,000.

Dk Kalemani alisema huo mradi utatoa huduma za kijamii kwa kuchangia katika ujenzi wa shule, vituo vya afya na viwanja vya michezo katika kaya zitakaozunguka mradi na wilaya za Malinyi, Ulanga, Morogoro Vijijini, Kibiti, Rufiji, Mlimba na maeneo mengine ya jirani.

Alisema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hutoa takriban Sh150 bilioni kwa mwaka kati ya hizo Sh66 bilioni huelekezwa kwenye huduma za jamii katika miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.

Dk Kalemani alisema mradi utakapokamilika utazalisha Megawati 2,100. Alisema umeme utakaouzwa kwa wateja utaingiza Sh1.6 trilioni kwa mwaka.

Alisema kulingana na usanifu, mradi unatarajiwa kudumu kwa miaka 80 tangu utakapoanza uzalishaji na kwamba, miradi mingine ya Kihansi na Mtera, uhai wake ni angalau miaka 50.

Kuhusu mpango wa kutunza mazingira, Dk Kalemani alisema Tanesco itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya uendelezaji mazingira kutokana na athari zinazoweza kujitokeza.

Uagizaji wa mafuta

Katika hotuba yake, Dk Kalemani pia alizungumzia Bandari ya Mtwara kuanza kupokea mafuta mwezi Juni kwa kutumia mfumo wa uagizaji kwa pamoja.

“Utaratibu wa kupanga bei ya mafuta yatakayoingizwa kupitia bandari hiyo utazingatia utaratibu unaotumika katika Bandari ya Tanga,” alisema.

Alisema miundombinu ya kuhifadhia mafuta iliyopo Tanga ina uwezo wa kutunza lita 26 milioni zinazotosheleza mahitaji ya ukanda huo kwa sasa.

Kuhusu usambazaji wa gesi asilia, alisema katika mwaka wa fedha 2018/19, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) litaweka miundombinu itakayowezesha zaidi ya nyumba 2,000 kuunganishiwa gesi asilia na kuisambaza katika mgahawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kampuni ya usimamizi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Udart) na kwa utekelezaji zimetengwa Sh20.9 bilioni.

Alisema mradi wa bomba la kusafirishia mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Uganda hadi Tanzania, umetengewa Sh54.2 bilioni, fedha za ndani kwa ajili ya kukamilisha majadiliano, usanifu wa kina wa kihandisi na kuwalipa wananchi watakaopisha mradi huo.

Alisema mradi huo utakaogharimu Sh8.07 trilioni hadi kukamilika ujenzi, unatarajiwa kuanza Juni na kukamilika mwaka 2020.