Mramba wa Tanesco sasa apiga injili kwa kwenda mbele

Muktasari:

Jana, kipeperushi kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kinaonyesha picha ya Mhandisi Mramba na maelezo kuwa atafundisha katika semina maalum ya Karama za Roho Mtakatifu na Utendaji wa Nguvu Kuu za Mungu.

Dar es Salaam. Aliyekuwa meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felschemi Mramba sasa amepata nafasi kubwa zaidi ya kutangaza injili baada ya uteuzi wake kutenguliwa.

Rais John Magufuli alimvua Mhandisi Mramba ukurugenzi wa Tanesco Januari mwaka huu baada ya shirika hilo kuwasilisha maombi ya kupandisha bei ya umeme. Nafasi yake ilichukuliwa na Dk Tito Mwinuka anayekaimu.

Katika maombi hayo kwa  Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Tanesco walitaka  bei ya umeme iongezwe kwa asilimia 8.5, lakini aliyekuwa Waziri wa Nishati, Profesa Sospeter Muhongo alikataa akisema hakushirikishwa na kwamba kukubali ni kinyume na sera ya kujenga viwanda.

Jana, kipeperushi kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kinaonyesha picha ya Mhandisi Mramba na maelezo kuwa atafundisha katika semina maalum ya Karama za Roho Mtakatifu na Utendaji wa Nguvu Kuu za Mungu.

 Kipeperushi hicho kinasema Mramba atafundisha  kuanzia Mei 30 hadi Juni 4 katika kanisa la Asemblies of God la Changanyikeni.

“Nimekuwa nikifanya hivyo siku nyingi, lakini sikuwa na muda. Sasa nina muda mzuri,” alisema Mramba alipozungumza na Mwananchi jana.

Mramba, ambaye kikazi bado yupo Tanesco, alisema amekuwa akijifunza neno la Mungu na anapolielewa hutaka kuwafundisha wengine, ingawa hajasomea uinjilisti au uchungaji.

“Najisomea vitabu vya dini, naandika vitabu pia. Kwa mfano nimeandika kitabu kuhusu roho mtakatifu, kuhusu Ayubu na kuhusu Juma la Pasaka,” alisema Mramba.     

 Mchungaji mwenyeji wa semina hiyo, Hossiana Muro alisema ni kweli Mhandisi Mramba amekuwa akifundisha katika semina mbalimbali ambazo zinaandaliwa na kanisa hilo.

“Atafundisha katika semina hiyo na ninawakaribisha sana,” alisema.

Hata hivyo, Mramba hakuwa tayari kuzungumzia kutenguliwa kwa Waziri Muhongo.

“Sina la kuzungumza,” alisema , akacheka na kukata simu.