Mamia wamzika Mtanzania aliyeuawa Uingereza

Muktasari:

Leyla amezikwa makaburi ya familia yao yaliyopo eneo la Sinoni katika jiji la Arusha.

 


Arusha. Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo, wameshiriki kumuaga na kumzika Mtanzania Leyla Mtumwa (36) anayedaiwa kuuawa na mume wake  nchini Uingereza.

Leyla, anadaiwa kuuawa usiku wa Machi 30 kwa kuchowma visu shingoni na kifuani na mume wake, Kema Kasambula katika nyumba yao.

Mwili wa Leyla uliwasili juzi Aprili 22 saa 12:00 jioni na ndege ya shirika la ndege la Qatar na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru.

Jana, Aprili 24 mwili ulipelekwa nyumbani kwao eneo la Kaloleni ambako uliswaliwa.

Gambo na mamia ya waombelezaji walijitokeza katika msiba huo, licha ya kuwapo mvua ambayo ilikuwa ikinyesha tangu majira ya alfajiri.

Mwili ulitolewa Hospitali ya Mount Meru, saa sita mchana na kuwasili nyumbani kwao saa saba mchana.

Baada ya mwili huo kufika kisomo maalumu kilifanyika na kuongozwa na Sheikh Rajabu Kihungiza.

Hata hivyo, katika msiba huo, Gambo hakuzungumza kwa maelezo kuwa hajakaa vyema kutokana na msiba wa mama yake, Rehema Mumburi ambaye alifariki dunia na kuzikwa wiki iliyopita Uru mkoani Kilimanjaro.

Leyla ameacha mtoto Tyrese Mtumwa (12). Mwanaume anayedaiwa kufanya mauaji hayo, Kasambula, anashikiliwa na polisi nchini Uingereza.