Msajili ataka wahuni kudhibitiwa

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Muktasari:

  • Kauli hizo ni sehemu ya mlolongo wa matukio yaliyotokea juzi baada ya watu wasiojulikana kuvamia mkutano wa viongozi wa CUF wilayani Kinondoni, kuwapiga na kuwatishia bastola, kabla ya  mmoja wao kudhibitiwa na wananchi.

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ametaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika katika vurugu hizo.

Kauli hizo ni sehemu ya mlolongo wa matukio yaliyotokea juzi baada ya watu wasiojulikana kuvamia mkutano wa viongozi wa CUF wilayani Kinondoni, kuwapiga na kuwatishia bastola, kabla ya  mmoja wao kudhibitiwa na wananchi.

Katika tukio jingine, uongozi wa CUF ulitinga Kituo Kikuu cha Polisi kuhoji hatua zilizochukuliwa baada ya shambulio hilo, huku Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa pole kwa waandishi wa habari na kulaani tukio hilo.

Wakati hayo yakitokea, wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wamemlaumu Msajili, ambaye ni mmoja wa washtakiwa katika kesi iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini wa CUF, wakisema hakupaswa kukaa kimya hadi baada ya vurugu kutokea.

Taarifa ya Jaji Mutungi aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari inasema ofisi yake haitasita kuchukua hatua stahiki kwa vyama vinavyokiuka sheria.

“Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika Hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es Salaam zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF,” alisema.