Msako wabaini Arusha kuna sukari na mafuta ya kula ya kutosha

Muktasari:

Msako huo umefanyika jana jijini humo

Arusha. Msako wa kamati ya ulinzi na usalama katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa umebaini kuwa jijini Arusha kuna mafuta na sukari ya kutosha hivyo ni marufuku kupandisha bei.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2018 baada ya msako huo jana, Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro amesema maghala yote ambayo wametembelea licha ya kuwapo uzalishaji mdogo wamebaini bado kuna mafuta na sukari.

"Kamati ya ulinzi na usalama wilaya imetembelea maghala na kuona bado kuna bidhaa na kwa sukari bado bei ya jumla mfuko wa kilo 50 ni kati ya Sh102,000 na Sh110,000,” amesema.

Amesema kutokana  na bei hizo bei ya kilo moja haipaswi kuuzwa zaidi ya Sh2,600 hivyo ambao watauza zaidi watachukuliwa hatua.

Daqarro amesema kuhusiana na sukari iliyofungwa bei pia haipaswi kuzidi Sh2,800 na taratibu zinafanywa kuhakikisha bei haiongezeki.

Kuhusiana na mafuta pia amesema yapo ya kutosha ikiwapo ya alizeti licha ya uzalishaji kupungua.

Wakizungumza na MCL Digital baadhi ya wakazi  wa Arusha waliomba Serikali kuendelea kudhibiti kupanda bei ya mafuta na sukari hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Jasmin Ally mkazi wa makao mapya amesema katika maduka mengi kati kati ya jiji sukari inauzwa kilo kati ya Sh2,700 na Sh2,800.

Hillal Kusena amesema bei ya mafuta na sukari inaendelea kupanda licha ya matamko ya Serikali.

"Serikali ingefatilia kujua tatizo ni nini kama ni kodi kubwa basi wapunguze lakini kutoa matamko tu hakutoshi," amesema Kusena.

Amesema bei ya mafuta ya kupikia bei ya jumla imepanda kutoka Sh 61,000 hadi Sh 70,000 kwa lita 20 huku lita 10 imepanda kutoka Sh 30,000 hadi Sh35,000.