VIDEO: Msamaha wa kodi taulo za kike wawakuna wengi

Muktasari:

Januari 22, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alipeleka hoja binafsi bungeni kuomba ipitishwe sheria ya kugawa bure taulo hizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Dar/Dodoma. Mapendekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango ya kufuta kodi kwa taulo za kike zinazoagizwa nje ya nchi, yamepokewa kwa furaha na watu mbalimbali wakiwamo wanaharakati, wabunge na wanawake.

Dk Mpango alitangaza mapendekezo ya msamaha huo jana, wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2018/19, “Napendekeza kusamehe VAT kwenye taulo za kike kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa bei nafuu kulinda afya ya mama na mtoto wa kike hasa walio vijijini na shuleni.”

Baada ya kutangaza msamaha huo Bunge lililipuka kwa shangwe na vigelegele hali iliyomfanya Spika Job Ndugai kumuomba waziri huyo arudie kipande hicho na akarudia.

Januari 22, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alipeleka hoja binafsi bungeni kuomba ipitishwe sheria ya kugawa bure taulo hizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, hoja hiyo ilikataliwa kutokana na kifungu kinacholikataza kujihusisha na kubadilisha kodi isipokuwa kupunguza.

Aprili wakati wa Bunge la Bajeti, Peneza aliuliza tena swali kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka kujua kama Serikali inaweza kuondoa kodi kwenye taulo hizo za kike.

“Kwa nini sasa Serikali kwenye sheria ya fedha inayokuja isiondoe kodi kwenye taulo hizi ili wanafunzi kutoka kaya maskini waweze kuzimudu?” alihoji Mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema Serikali ina utaratibu wake wa kuondoa kodi kwenye bidhaa zinazoleta tija.

“Wizara ya Fedha na Tamisemi wataona namna watakavyokaa kwa pamoja kuona jinsi ya kupunguza bei kwenye vifaa ulivyoeleza,” alisema.

Baada ya mapendekezo ya Waziri Mpango jana, Peneza aliishukuru Serikali kwa kufuta kodi hiyo akisema ni ishara kwamba Serikali imesikia maoni ya wadau mbalimbali.

Alisema kinachopaswa kufanywa sasa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujipanga kufuatilia ili kuhakikisha zinapatikana kwa gharama nafuu.

“Kwa kuwa kodi imefutwa, matarajio yangu ni kwamba, idadi ya watumiaji wa pedi itaongezeka, kwa hiyo niombe TRA ijipange ili zipatikane kwa bei ya chini na kwa wingi,” alisema Peneza.

Mwanaharakati wa masuala ya jinsia aliyewahi kuhamasisha ugawaji wa taulo hizo bure kwa wanafunzi, Rebeca Gyumi aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo hususan kwa waziri mwenye dhamana ya afya, Ummy Mwalimu.

Alisema hatua hiyo imeonyesha kuwa sasa wanaelekea walikokuwa wanatakiwa kufika.

“Naomba mambo mawili yafanyike, moja Serikali kusimamia ili kuhakikisha wazalishaji wanapunguza bei,” alisema.

Pili kuhakikisha zinafika vijijini ambako mahitaji ya taulo hizo ni makubwa.

Wengine waliopongeza hatua hiyo ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mohammed Enterprises, Mohammed Dewji ambaye ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

“Serikali imeondoa kodi kwa taulo za kike, ili kurahisisha upatikanaji kwa wanawake na wasichana, hasa maeneo ya vijijini. Ninapongeza uamuzi huu.”

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Kuondolewa kwa kodi kwenye taulo za kike ni mwanzo mzuri. Rebecca Gyumi na Upendo Peneza, juhudi zenu zimezaa matunda.”