Kamati Kuu ya Chadema yasogezwa mbele saa 24 zijazo

Muktasari:

Kamati Kuu ya Chadema iliyokuwa imepangwa kufanyika leo imeahirishwa hadi kesho.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema iliyokuwa imepangwa kufanyika leo imeahirishwa hadi kesho.

Kikao hicho kimeahirishwa ili kutoa fursa ya viongozi na wanachama wa Chadema kushiriki mazishi ya Anna Mayunga ambaye ni mama wa mkurugenzi wa sheria wa chama hicho, , Peter Kibatala.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamisi Januari 13, 2018, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema “ni kweli Kamati Kuu ilikuwa ikutane leo lakini imeahirishwa hadi kesho(Jumapili).”

“Tumeahirisha ili kutoa nafasi ya viongozi kushiriki mazishi ya mama yake Kibatala yanayofanyika leo(Jumamosi) Morogoro mjini na Kamati Kuu itakutana kesho(Jumapili) jijini Dar es Salaam.”

Mrema amesema marehemu Anna alifariki juzi Alhamisi baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliokuwa amejikinga na mvua zilizokuwa zikinyesha na kudai kwamba si pekee aliyefariki kuna wengine pia.

Amesema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe tayari yupo mkoani Morogoro kuhudhuria mazishi hayo akiwa pamoja na viongozi wengine na wabunge.