Msimamo wa Mtaka wawakuna CCM, Chadema

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka


Muktasari:

Kuwaweka rumande viongozi hao si njia sahihi ya kutatua matatizo

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewakosoa viongozi ambao wamekuwa na hulka ya kuwaweka rumande watumishi umma na wanasiasa akisema, “Katika mkoa wangu hutoona huo upuuzi.”

Katika msimamo huo ambao umeungwa mkono na viongozi wa CCM, Chadema na wanaharakati, Mtaka amesema kuwaweka rumande viongozi hao si njia sahihi ya kutatua matatizo yanayowazunguka wananchi huku akitaka mamlaka za kinidhamu ziheshimike na kuzingatiwa na si vinginevyo.

Mtaka ametoa kauli hiyo kipindi ambacho wimbi la wakuu wa wilaya (ma-DC) kuwaweka rumande watumishi wa umma walio chini yao, wabunge na madiwani kwa tuhuma mbalimbali likikithiri.

Kwa kauli hiyo, Mtaka anaungana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na aliyekuwa waziri wa Tamisemi, George Simbachawene kukemea matumizi mabaya ya amri hiyo.

Kauli ya karibuni zaidi imetoka kwa Waziri Jafo ambaye akizungumza na wakuu wapya wa wilaya jijini Dodoma alisema tabia hiyo inasababisha wananchi kuichukia Serikali na kuwaagiza waitumie ilivyokusudiwa na si kuonea watu, akiwataka kuzisoma sheria zinazowaongoza ili wafanye kazi kwa weledi.

Mei mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuzingatia mipaka ya madaraka yao na kuhakikisha hatua wanazochukua katika utendaji wao zinafuata sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma.

Aidha, Septemba 25 mwaka jana, Waziri Ummy akizindua majengo ya wodi ya wazazi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, alikemea wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka ndani watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma.

Mwishoni mwa wiki, Mtaka akifunga semina ya madakatari wa mikoa, wilaya na wadau wa sekta ya afya iliyofanyika jijini Dodoma, aliwataka viongozi kuwalinda watumishi wa ngazi ya chini na kubainisha kwamba Simiyu hakuna suala la mtumishi kupelekwa rumande.

“Sisi ambao ni viongozi katika sekta hii, kwanza tuwalinde watumishi wetu, mimi nilipokwenda kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu niliwaambia ma DC, moja ya jambo ambalo sitaki kulisikia ni mtumishi yeyote wa umma kuwekwa lokapu,” alisema.

Huku akishangiliwa na watumishi hao wa sekta ya afya, Mtaka alihoji, “Huyo anayemweka ndani mwenzake, ikitokea kinyume chake angefurahia suala hilo?”

Alisema hakuna aliyezaliwa anajua na kama kuna kiongozi anaona mtumishi mwenzake hajui ni wajibu wake kumpa mafunzo na si kumchukulia hatua za kumweka ndani.

“Wakati mwingine ukiona matamko ya wanasiasa kule kwenye maeneo yenu ya kazi unajiuliza hivi huwa anakaa kushauri haya yatokee, nazungumza ‘with prestige’ (kwa ufahari) kwa sababu katika mkoa wangu hutoona huo upuuzi,” alisema Mtaka.

Akifafanua kauli hiyo jana alipozungumza na Mwananchi, Mtaka alisema kuna makosa madogo ambayo yanajitokeza ambayo wakuu wa wilaya au mikoa wangeweza kuyamaliza kwa kufuata taratibu za utumishi wa umma.

Alisema kumekuwapo na matukio ya watumishi kuwekwa ndani yanayoshusha molari kwa watumishi.

“Mamlaka ya kinidhamu kwa kila mtumishi zipo na hazipaswi kupuuzwa, zipo namna ya kufanya daktari, mwalimu, ofisi elimu, polisi wanapokosea lakini si kupelekwa polisi,” alisema Mtaka.

“Hivi baada ya kumweka ndani na kutoka kipi kinafuata? Ukitumia mamlaka vibaya huwezi kupata matokeo,” aliongeza, “Kama ni kiongozi unasimamia misingi ya utumishi wa umma? Sisi tunasema huwezi kujenga uchumi wa kipolisi katika mikoa.”

Alisema si watumishi wa umma pekee, bali hata wanasiasa wakiwamo wabunge na madiwani hawapaswi kuwekwa ndani ovyo, “Ukimaliza kuwaweka watumishi wa ndani wakaisha, mtaanza kuwekana wenyewe, huoni kuna wabunge wa CCM nao wanalalamika! Kwa maana watu wa kuweka ndani wameisha mnaanza kuwekana wenyewe na mwisho wa siku unabaki wewe mwenyewe.”

Alisema katika utumishi kuna eneo la mkuu wa mkoa, wilaya, mbunge na diwani ambao kwa pamoja wanapaswa kushirikiana ili kufikia azma ya dira ya Taifa ya maendeleo na vipaumbele vya Rais John Magufuli.

Awakuna Polepole na Sugu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipotakiwa kutoa maoni yake juu kauli hiyo ya Mtaka alisema, “Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria tuliziojiwekea na huu ndio msimamo wa CCM na Rais John Magufuli anasimamia hilo.”

Polepole alisema, “Viongozi wanaofanya kazi CCM au serikalini kwa niaba ya CCM wanapaswa kuheshimu Katiba, sheria na taratibu nzuri. Wachape kazi zaidi kwa sababu muda haututoshi.”

Akitoa maoni yake, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema, “Nampongeza sana Mtaka na hao ndio viongozi au wasaidizi wanaopaswa kumsaidia Rais. Mtaka amekuwa mtu anayeshauri kwani unapokuwa na viongozi wanaowaweka ndani watumishi wa chini inasababisha kushuka kwa morali ya kufanya kazi.”

Sugu alisema mtumishi wa umma anapokosea kuna taratibu za kinidhamu na si kuwekwa ndani jambo ambalo halina tija.

“Kama mtu amekosea kwa nini asiwajibishwe kwa sheria za utumishi? Kwa hiyo alichokisema Mtaka ni kweli kabisa na watendaji wote mawaziri, wakuu wa mikoa wawe kama Mtaka,” alisema Sugu.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za BInadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema, “Tunampongeza sana RC Mtaka na wengine wanapaswa kujitokeza na kukemea vitendo hivi kama alivyofanya Waziri Jafo.”

Alisema matumizi ya kumweka ndani mtu saa 24 au 48, “Yalilenga kipindi cha ukoloni na kwa mtu anayetishia amani, sasa hivi mtu anawekwa ndani kwa kuchelewa au kusimamia mradi visivyo jambo ambalo anaweza kushughulikiwa kwa taratibu za kinidhamu.

“Umefika wakati sasa tukaacha tu kusema na tukaenda kubadili hiyo sheria ambayo imekuwa haitumiki visivyo lakini kwa ma RC na DC wanapaswa kufuata nyayo za Mtaka ambaye amekuwa RC anayejali na kusimamia misingi ya utawala bora,” alisema Ole Ngurumwa.