Msimamo wa Serikali ya Tanzania uuzaji Airtel uliwavyoibua watalaamu

Muktasari:

Kampuni ya Airtel Africa imetangaza kuuza hisa za awali (IPO) katika Soko la Hisa London (LSE) lakini Serikali imesema mpango huo ni batili kwa sababu majadiliano ya umiliki wa hisa za Airtel Tanzania bado yanaendelea. Wataalamu wa masuala ya fedha na uwekezaji wamefafanua.

Dodoma. Wataalamu wa masuala ya fedha na uwekezaji wamesema msimamo wa Serikali kupinga mpango wa kampuni ya Airtel Africa kuuza hisa zake za awali (IPO) katika Soko la Hisa London (LSE), Uingereza utasaidia kuharakisha kutafuta suluhu nchini.

Airtel Africa inajipanga kufanya IPO Septemba mwakani ikitarajia kuongeza Dola 8 bilioni za Kimarekani zitakazosaidia kuimarisha operesheni zake kwenye nchi 14 za Afrika pamoja na kulipa deni lake linalofika Dola 5 bilioni.

Akizungumza na wanahabari leo, Oktoba 31, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema mpango huo ni batili nchini kwamba uamuzi wowote wa kuuza au kuhamisha hisa au ukaribishaji wa wanahisa wapya unapaswa kuishirkisha Serikali.

Mkurugenzi wa fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wilfred Luyangi anasema kukamilisha mchakato wa kuorodheshwa kwake LSE, Airtel Africa itatakiwa kuwasilisha taarifa za operesheni za matawi yake yote ikiwamo Tanzania. “Kabla ya kuorodheshwa lazima kampuni husika iwasilishe hesabu zake za fedha kutoka kwenye kila tawi. Huko, Airtel Tanzania itatajwa tu. Kwa taarifa ya Serikali, Bharti Aitrel lazima waje kumaliza utata uliopo,” anasema Luyangi.

Serikali ina mgogoro wa umiliki wa hisa za Airtel Tanzania na kampuni mama yake yenye makao makuu yake nchini India, Bharti Airtel suala linalofanyiwa majadiliano hivi sasa.

Kwa taarifa zilizopo sasa zinaonyesha Serikali inamiliki asilimia 40 wakati Bharti Airtel ikiwa nazo asilimia 60 ya hisa za Airtel Tanzania lakini Serikali inasema yenyewe inamiliki asilimia zote kwa kuwa uuzaji wa hisa hizo ulikiuka sheria na utaratibu.

Endapo suluhu ya haraka haitopatikana na Airtel Africa ikaamua kupuuzia mgogoro uliopo nchini na kuamua kujisajili kwenye soko hilo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema inaweza kupata hasara.

“Bila kujali udogo wa Airtel Tanzania, uorodheshaji wa Airtel Africa utaihusisha Tanzania ambayo ina mgogoro wa hisa na kampuni mama. Kinachotakiwa ni kuumaliza mgogorouliopo kwanza vinginevyo bei ya hisa itakuwa ndogo sana,” anasema.