Msimu mpya wa pamba na mambo mapya

Muktasari:

Katika msimu mpya utaratibu wa kununua pamba kwa mkulima mmoja mmoja umepigwa marufuku.

Wakati Mei Mosi ikitangazwa kuwa siku rasmi ya kuanza msimu wa ununuzi wa zao la pamba, mfumo na utaratibu wa kununua zao hilo pia umebadilishwa msimu huu.

Badala ya mfumo na utaratibu uliozoeleka wa kila mnunuzi kununua pamba kutoka kwa mkulima moja kwa moja shambani, msimu huu pamba yote itanunuliwa kupitia vyama vya ushirika vya wakulima.

Hayo ni baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha wadau wa sekta ya pamba kinachoendelea jijini Mwanza leo Februari 21 chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kikao hicho kinachoendelea kinahudhuriwa na wadau wakiwemo wakulima, wanunuzi na wamiliki wa vinu vya kuchambua pamba, watendaji kutoka Bodi ya Pamba nchini (TCB), wataalam wa kilimo, taasisi za fedha, wawakilishi wa kisiasa na wakuu wa mikoa na wilaya zinazolima zao hilo kutoka Mara, Geita, Simiyu, Tabora na wenyeji Mwanza.

Pendekezo la msimu wa ununuzi wa pamba kuanza Mei Mosi badala ya Juni iliyotolewa na Serikali na kuungwa mkono na wadau unalenga kuwaondolea wakulima wanaovuna mapema adha ya kuendelea kuhifadhi mavuno yao kwa muda mrefu kusubiri msimu kuanza.

Kuhusu bei ya ununuzi msimu huu, Waziri Mkuu amewataka wadau wa zao hilo kusubiri hadi msimu utakapokaribia kwa sababu upangaji unategemeana na bei kwenye soko la dunia.

 

Mwenyekiti wa wafanyabiashara na wanunuzi wa pamba, Christopher Gachuma amesema wao (wafanyabiashara na wanunuzi), hawana pingamizi kuhusu tarehe ya kuanza msimu wa ununuzi wala utaratibu wa pamba kununuliwa kupitia vyama vya ushirika akisema utawapunguzia gharama za kuzunguka kwenye mashamba ya wakulima.

 

“Mfumo wa zamani wa kununua moja kwa moja kwa wakulima ulitulazimisha kuajiri watu wengi ambao baadhi yao walifanya udanganyifu na hivyo kutusababishia hasara; mfumo huu mpya utatupunguzia gharama,” amesema Ghachuma.

 

Ameiomba Serikali Kuu kuingilia kati na kuzuia maagizo ya baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wanaowalazimisha wafanyabiashara kulipa fedha taslimu za makadirio ya kilo za pamba wanazotarajia kununua kabla ya kuanza zoezi la ununuzi.

"Tunaomba pia kupata ufafanuzi kuhusu kiwango cha malipo ya ushuru wa mazao kwa sababu mara tunaambiwa ni asilimia tatu na wakati mwingine tano,” amesema Ghachuma.

Akijibu suala la wafanyabiashara kulazimishwa kulipa fedha taslimu kabla ya kujua kiasi cha kilo za pamba atakazonunua, Waziri Mkuu amepiga marufuku suala hilo na kuwaagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuzingatia utaratibu wa malipo ya fedha za Serikali.

“Ni marufuku kuchukua fedha yoyote kabla ya kujua kiasi gani cha pamba kipo na kitanunuliwa,” ameagiza Majaliwa.

Akizungumzia matarajio ya mavuno msimu huu, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amesema zaidi ya kilo 600 milioni zinatarajiwa kulinganisha na kilo 133 milioni za msimu wa ununuzi uliopita.

Pamoja na kuimwagia sifa Bodi ya Pamba nchini (TCB), na wadau wengine kwa jitihada zilizofanyika kuongeza tija kwenye sekta ya pamba, Waziri Tizeba ameiagiza bodi hiyo kusimamia kwa makini na ukaribu hatua zilizosalia kuhakikisha tija na ubora utakaoipa soko pamba ya Tanzania kwenye soko la dunia.

Tizeba amesema wizara imemwagiza mrajisi wa ushirika kuhakikisha maofisa ushirika wanaenda katika halmashauri zote zinazolima pamba kusimamia zoezi la kupatikana kwa viongozi wa vyama vya msingi vitakavyonunua pamba kutoka kwa wakulima.