Msudani aliyekamatwa na dola 60,000 JNIA apandishwa kizimbani

Raia  wa Sudan, Nada Zaelnoon Ahmed Elbokhary(38)( aliyeandika uso na Mtandao mwekundu) akitoka katika cha chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kukutwa na dola za kimarekani 60,000 katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl Julius Nyerere(JNIA) ambazo hajazitolea taarifa kwa Mamlaka husika.

Muktasari:

Raia wa Sudan, Nada Zaelnoon Ahmed amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la kukutwa na dola za kimarekani 60,000 pamoja na fedha za Sudan paundi  3,410 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere,  ambazo hajazitolea taarifa  mamlaka  husika

Dar es Salaam. Raia  wa Sudan, Nada Zaelnoon Ahmed Elbokhary (38) leo Oktoba 15, 2018 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kukutwa na dola za kimarekani 60,000 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA) ambazo hajazitolea taarifa kwa mamlaka husika.

Elbokhary ambaye ni mkazi wa Masaki jijini,  ametakiwa, kujibu shtaka moja la kushindwa kutolea taarifa ya fedha hizo kwa Mamlaka ya Forodha.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amedai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Oktoba 9, 2018 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo katika wilaya ya Ilala jijini.

Mwita amesema siku hiyo, mshtakiwa Elbokhary wakati akiondoka Tanzania kuelekea Sudan, alikutwa akiwa na dola za Marekani 60,000 ambazo ni zaidi ya Sh.120 milioni na paundi 3,410 za Sudan ambazo hakuzitolea maelezo kwa mamlaka ya forodha.

Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Hakimu Simba ametoa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa  na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaosaini bondi ya Sh 20 milioni kila mmoja.

Pia mahakama hiyo imemtaka mshtakiwa huyo kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani hapo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 22 Mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).

Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande.