Msukuma asema wametishwa na kifo cha mmiliki wa mabasi

Muktasari:

Akizungumza jana kwa niaba ya wenzake wakati wa ibada ya mazishi ya mmiliki huyo mabasi ya Super Sammy iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Majengo Mapya mjini Magu, mmiliki wa mabasi ya Msukuma, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ alisema tukio hilo limewafanya wajihisi kuwa yeyote miongoni mwao anaweza kufuata kutekwa na kuuawa.

Magu. Wamiliki wa mabasi mkoani Mwanza, wamesema kwamba wameingiwa na hofu ya usalama wa maisha yao baada ya mwenzao Samson Josia kupotea katika mazingira ya kutatanisha na baadaye mwili wake kukutwa ukiwa umefungwa kwenye viroba na kutupwa ndani ya Mto Mandaka.

Akizungumza jana kwa niaba ya wenzake wakati wa ibada ya mazishi ya mmiliki huyo mabasi ya Super Sammy iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Majengo Mapya mjini Magu, mmiliki wa mabasi ya Msukuma, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ alisema tukio hilo limewafanya wajihisi kuwa yeyote miongoni mwao anaweza kufuata kutekwa na kuuawa.

“Wamiliki na wafanyabiashara wa mabasi tumejawa hofu kwa tukio lililomkumba mwenzetu; hatujui nani anafuata baada ya Super Sami. Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike kuwabaini na kuwatia mbaroni waliohusika,” alisema Msukuma ambaye pia ni mbunge wa Geita Vijijini

Akitoa salamu za Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Ofisa Habari wa chama hicho, Mustapher Mwalongo licha ya kukabidhi ubani wa Sh3 milioni kwa familia ya marehemu, alisema Taboa itashirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Pia, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya, Renatus Ng’hula alisema mauaji ya aina hiyo yanachafua haiba na taswira ya Taifa, “Tumekuwa tukisoma na kuona matukio haya kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; leo imefika kwetu kwa mtu tuliyemtegemea kwenye masuala mengi ya kiuchumi na maendeleo.”

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mazishi, kiongozi wa ukoo wa Mzuri, Yusufu Kijika alisema wauaji licha ya kumchinja marehemu, pia walikata na kutenganisha na kiwiliwili miguu yote miwili.

Alisema ingawa bado uchunguzi unaendelea, wanahusisha mauaji hayo na madeni ambayo marehemu alikuwa akiwadai watu mbalimbali walioshindwa kurejesha, “Tunahisi ukaribu na moyo wake wa kusaidia wengine kupitia mikopo ndicho kimemponza; marehemu alikuwa hadaiwi na mtu, bali yeye ndiye alikuwa akiwadai aliowakopesha.”

Alisema saa chache kabla ya kutoweka, Samson alimpigia simu mmoja wa wake zake, Stumai Magembe akimwagiza kuandaa chakula cha kutosha na sehemu ya kulala wageni aliosema angefika nao kwenye mji wake mwingine ulioko jijini Mwanza.

“Kwa mujibu wa Stumai, simu hiyo alipigiwa saa 3:45 usiku wa Februari 27; lakini baada ya simu hiyo, marehemu hakuonekana wala kupatikana kwenye simu hadi mwili wake ulipokutwa Mto Ndabaka siku tano baada ya gari lake kukutwa likiwa limeteketezwa kwa moto katika Hifadhi ya Serengeti,” alisema

Alisema familia ilifanya jitihada na kubaini kuwa wakati anapiga simu usiku huo, alikuwa eneo la Buzuruga jijini Mwanza na kwamba mawasiliano ya mwisho yalionekana akiwa hifadhi ya Serengeti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed alisema jana kuwa watu wanaoshikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio hilo imefikia watano baada ya mwingine kuongezeka juzi jioni.

Katika tukio lingine, mmoja wa waombolezaji waliokuwa msibani hapo, alitiwa mbaroni na baada ya ndugu wa marehemu kumtambua kuwa alifika nyumbani hapo siku ambayo Samson alipotea akimuulizia na kuondoka bila kueleza alichokuwa akimtafutia licha ya kuulizwa.

Mwili wa mfanyabiashara huyo ulikutwa ndani ya mto siku tano baada ya gari yake ndogo aina ya Toyota Land Cruiser kukutwa ikiwa umeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Baadaye mwili wake uliokotwa na wavuvi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao ndani ya mto huo Machi 14.