Mswada wa sheria ya fedha kuleta maumivu zaidi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Katika muswada huo wa fedha uliowasilishwa juzi bungeni, yapo mapendekezo kadhaa yanayolenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato kufanikisha matumizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Dodoma. Wafanyabiashara wadogo, wachimbaji wadogo wa madini na waendeshaji wa taasisi za kujitolea (NGOs) watakuwa na wakati mgumu baada ya Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya 2017/18.

Katika muswada huo wa fedha uliowasilishwa juzi bungeni, yapo mapendekezo kadhaa yanayolenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato kufanikisha matumizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Bunge linaendelea na mjadala wa bajeti ya Serikali unaotarajiwa kumalizika wiki ijayo na baadaye kuujadili muswada huo.

Sehemu ya nne ya muswada inapendekeza kuifanyia Marekebisho Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Marekebisho yanayotarajiwa kufanyika kwenye kifungu cha 37 ili kuwatambua wafanyabiashara wadogo wanaofanya kazi katika maeneo yasiyo rasmi.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo itakuwa lazima kwa wafanyabiashara hao kuwa na vitambulisho kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipowasilisha makadirio na matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Endapo muswada huo utapitishwa kama ambavyo inatarajiwa, watakaoshindwa kufanya hivyo, watatakiwa kulipa faini au kutumikia kifungo gerezani. Adhabu hizo zimeainishwa katika kifungu cha 67 kinachopendekezwa kuandikwa upya ili kuongeza adhabu kwa atakayekiuka masharti ya sheria hiyo.

Wafanyabiashara hawa ambao awali hawakuwa na adhabu yoyote ya kisheria, inapendekezwa walipe faini isiyopungua Sh200,000 na isiyozidi Sh1 milioni au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka miwili.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema halikuwa lengo la Bunge kuwaadhibu wafanyabiashara ndogondogo isipokuwa kuwahamasisha kurasimisha shughuli zao, lakini kwa mapendekeo hayo, hali itakuwa tofauti.

“Adhabu zilizopendekezwa zitapunguza morali kwa wafanyabiashara hawa kujisajili,” alisema mbunge huyo.

“Ipo tabia ya kuonyesha bajeti ni nzuri kumbe ni kinyume chake. Serikali ilipaswa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari badala ya kutunga sheria kali.”

Nafuu watakayoipata wafanyabiashara hao ni ushuru wa usafi sokoni ambao unapendekezwa kufutwa. Kwa wauzaji wa nyama, watarajie kufutiwa ada za vibali vya machinjio.

Taasisi zisizo za Serikali

Pia, sehemu ya kumi ya muswada huo inapendekeza kutungwa kwa Sheria itakayoweka masharti katika kuweka, kutoza au kubadilisha baadhi ya kodi, tozo au ada. Vilevile, inapendekeza kurekebisha sheria nyingine zinazohusu ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya umma.

Sehemu ya tatu ya muswada huo, inawagusa wengi ambao watatakiwa kuhakikisha wanabadili mazoea. Mabadiliko yanayopendekezwa yanawagusa wachimbaji wadogo wa madini, kampuni zinazopata hasara, NGOs na wasafirishaji wa maua nje ya nchi.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyomo ni pendekezo la kuboresha kifungu cha 64 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuanza kutoza kodi taasisi za kujitolea ambazo awali zilikuwa nje ya utaratibu huu.

Taasisi hizo zinazotegemea mapato kutoka kwa wafadhili kwa kiasi kikubwa, zitalazimika kutenga sehemu ya wanachopokea kwenda hazina ya Serikali kwa ajili ya Watanzania wote.

Wachimbaji wadogo wa madini wamepewa nafasi ya kuchangia mapato ya taifa. Baada ya mvutano wao wa muda mrefu na wawekezaji wa madini, muswada unapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 83B ili kuweka kodi ya zuio kwenye mauzo ya madini ya wachimbaji wadogo na wa kati.

Mabadiliko ya Sheria hiyo ya mapato yanatoa ahueni kwa wasafirishaji wa maua nje ya nchi. Mabadiliko yanayopendekezwa ni kufanya marekebisho ya vifungu vya 90 ili kuleta unafuu wa gharama za usafirishaji wa maua kwa ndege.

Madini

Baada vita vilivyoanzishwa na Rais John Magufuli kudhibiti wizi na udanganyifu unaofanywa katika sekta ya madini, Bunge linatarajia kubadilisha kifungu cha 18 cha Sheria ya Madini ili kuzuia uuzwaji nje ya nchi.

Sehemu ya tano ya muswada huo, inapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 90 ili kuweka asilimia moja ya ada ya ukaguzi kwenye madini kabla ya kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi.

Marekebisho yatakayofanyika kwenye kifungu cha 112 cha sheria hiyo kinatarajia kumpa waziri anayehusika mamlaka ya kutengeneza kanuni za ukaguzi na utozaji wa ada kwa wasafirishaji.

Kodi ya majengo

Kuanza kukusanywa kwa kodi ya majengo na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kunampa mamlaka Waziri wa Fedha kutambua notisi za madai zitolewazo na TRA.

Mamlaka hayo yatapatikana endapo mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Kodi ya Mamlaka za Miji yaliyopo kwenye sehemu ya tisa ya muswada huo, yatapitishwa.

Marekebisho haya yanalenga kubainisha kiwango cha tozo kwa nyumba ambazo hazijafanyiwa tathmini na TRA kwa mujibu wa sheria ya Kodi za Jengo.

Mapendekezo hayo yakiridhiwa, Wizara ya fedha itaruhusiwa kutoza kodi hiyo kwa nyumba zote zilizopo mjini. Mpango wa bajeti unapendekeza tozo ya Sh10,000 kwa nyumba ya kawaida ambayo haijafanyiwa tathmni na Sh50,000 kwa ghorofa la namna hiyo.