Mtaalamu wa kodi awa Gavana

Rais John Magufuli akimtunuku Profesa Florens Luoga cheti cha pongezi na shukrani katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Rais Magufuli aliwatunuku vyeti hivyo wajumbe wa kamati maalumu za uchunguzi na majadiliano kuhusu rasilimali za madini nchini. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Profesa Luoga, ambaye alikuwa mjumbe wa kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza sakata la makinikia, anakuwa Gavana wa saba tangu nchi ipate uhuru na anachukua nafasi ya Profesa Benno Ndulu anayemaliza muda wake Januari 7, mwakani.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amepiga hatua nyingine katika jitihada zake za kukusanya na kudhibiti mianya ya kodi baada ya kumteua msomi aliyebobea katika sekta hiyo, Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT).

Profesa Luoga, ambaye alikuwa mjumbe wa kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza sakata la makinikia, anakuwa Gavana wa saba tangu nchi ipate uhuru na anachukua nafasi ya Profesa Benno Ndulu anayemaliza muda wake Januari 7, mwakani.

Profesa Ndulu, aliyefanikiwa kushusha mfumuko wa bei, alipokea nafasi hiyo kutoka kwa Dk Daudi Ballali aliyehudumu kati ya mwaka 1998 mpaka Januari 8, 2008 kabla ya kutimuliwa kutokana na sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Malipo ya Nje (Epa).

Mwanasheria huyo aliyebobea katika masuala ya kodi, anapewa nafasi hiyo wakati Serikali ya Tano ikipambana vikali na wakwepa kodi, kampuni za nje katika mapato yatokanayo na madini, na kuongeza wigo wa kodi, huku Rais Magufuli akiongoza vita anayoiita ya kiuchumi.

Rais Magufuli alitangaza uteuzi huo jana baada ya kuwatunukia vyeti wajumbe wa kamati mbili alizoziunda kuchunguza biashara ya madini, sheria, mikataba na usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi.

Pia amemtunuku cheti Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuonyesha uzalendo wake baada ya kupokea mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria za rasilimali za Taifa na kuruhusu Bunge lijadili na kupitisha kwa hati ya dharura.

“Profesa Ndulu amefanya kazi nzuri sana na anamalizia muda wake. Nafikiri mwezi wa 12 au wa kwanza anatakiwa amalize hiyo kazi. Imebaki miezi kama miwili hivi,” alisema Rais.

“Anatakiwa awe anaanza ku-handle (anakabidhi) kwa yule nitakayemteua. Na mimi kwa ku- appreciate kazi hii ilivyofanywa vizuri, nimeamua pia kumteua Gavana wa Tanzania miongoni mwa hawa niliowapa vyeti leo. Sijui nimtaje hapa hapa?” alisema Rais huku akipigiwa makofi.

“Ili watu wazuri waanze kupata hivyo hivyo, ninataendelea hivyo hivyo, lakini nataka niwaeleze nimemchagua Profesa Luoga ndiye atakuwa Gavana wa Tanzania mara baada ya Gavana aliyepo kukabidhi rasmi. Na kwa sababu nimezungumza hivi, nina uhakika Gavana aliyepo atafanya haraka haraka kumkabidhi.”

Rais Mgufuli alisema anatambua uwezo wa Profesa Luoga, ambaye ni makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika masuala ya kodi, akisema eneo hilo ndilo lilikuwa linasumbua Taifa.

“Tulikuwa tuna upungufu pale kwenye taxation (utozaji kodi) na ndiyo tumechezewa sana. Huyu ni mtalaamu wa taxation kwa hiyo hao wanaoleta pesa wanafungua akaunti mahali fulani watakwama kwa sababu walikwama walipokuwa kwenye mijadala yao. Luoga oyeee,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa kwa makofi ukumbini hapo.

Profesa Luoga ana shahada ya uzamivu ya Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza na amekuwa akifanya utafiti na kuandika machapisho kuhusu kodi kwa ajili ya wanafunzi na wasomi.

Miongoni mwa kazi zake ni A Sourcebook of Income Tax Law in Tanzania, ambacho kinazungumzia Sheria ya Kodi ya Mapato na ni kwa ajili ya wanafunzi wa fani hiyo. Chapisho lake jingine ni The Viability of Developing Democratic Legal Frameworks for Taxation in Developing Countries: Some Lessons from Tanzanian Tax Reform Experiences, ambacho kinazungumzia umuhimu wa uwazi na demokrasia katika utozaji kodi kwa nchi zinazoendelea kwa kutumia mfano wa Tanzania.

Kabla ya kutangaza uteuzi huo, Rais Magufuli aligusia suala la sheria ambazo zimekuwa hazitumiki. Rais alitumia mfano wa Sheria ya Mwaka 1992, inayosimamia fedha za nje.

“Fedha ambazo tumekuwa tukipoteza ni nyingi. Tumekuwa na sheria ambazo wakati mwingine tumekuwa hatuzitumii na ndiyo maana yamekuwa yakija makampuni hapa yanafungua akaunti kwenye nchi ambazo zimekuwa hazitozi kodi na sisi tunaruhusu wakati sheria hairuhusu,” alisema Rais.

“Huwa naizungumzia BoT, kwa nini haikuzuia haya mambo? Kwa nini waliruhusu? Hata baada ya hawa kutengeneza faida yao mwaka 2009, kwa nini hawakuwaleta hapa wawe registered (wasajiliwe) ili tujue fedha wanazoingiza? Lakini saa nyingine ukizungumza watu wakasema ninamsema fulani.”

Licha ya Profesa Ndulu kutoguswa na kashfa zilizoikumba nchi, hasa ya uchotwaji wa fedha kutoka Akaunti ya Escrow iliyokuwa BoT, Rais Magufuli amekuwa akionekana kukerwa na utendaji wa BoT, kwa madai ya kutosimamia ipasavyo rasilimali za Taifa pamoja na udhibiti wa matumizi ya fedha.

Akizungumzia uteuzi wake, Profesa Luoga amesema amepokea kwa heshima kubwa dhamana aliyopewa na Rais Magufuli na kwamba anatambua changamoto za nafasi hiyo na kuahidi kutumia wataalamu.

“Nimepokea kwa heshima dhamana niliyopewa nikitambua kwamba zipo changamoto. Nitakwenda kujifunza zaidi. Kwa sababu sijawahi kuwa Gavana, nitatumia wataalamu waliopo,” alisema.

Julai 11, Rais Magufuli alimteua Profesa Luoga kuwa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato(TRA) akichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Novemba mwaka jana na bodi hiyo kuvunjwa.

Nyongeza na Kelvin Matandiko