Mtangazaji Maribe, Irungu kukaa mahabusu wiki

Muktasari:

  • Jumatano, Jaji James Wakiaga aliagiza ofisi ya uangalizi kuandaa na kuwasilisha ripoti ya awali mahakamani kabla siku ya kusikilizwa dhamana Oktoba 24.

Nairobi, Kenya. Mtangazaji wa televisheni Jacque Maribe na mpenzi wake Joseph Irungu bado wataendelea kukaa mahabusu kwa wiki moja zaidi baada ya mahakama kupanga siku ya kusikiliza maombi yao ya dhamana kuwa juma lijalo.
Jumatano, Jaji James Wakiaga aliagiza ofisi ya uangalizi kuandaa na kuwasilisha ripoti ya awali mahakamani kabla ya siku ya kusikilizwa dhamana Oktoba 24.
Ripoti ya wafanyakazi jamii itajulisha uamuzi wa jaji wakati wa kuamua ikiwa awanyime dhamana au la.
Hata hivyo, ni mashtaka ambayo yanapaswa kuishawishi mahakama kwamba kuna sababu za kulazimisha kukataa dhamana kwa watuhumiwa wa mauaji.
Wawili hao wanashtakiwa kwa kuhusika kumuua mfanyabiashara wa kike Monica Kimani usiku wa Septemba 19 nyumbani kwake katika ghorofa ya Lamuria Gardens, Kilimani.
Mahakama ilielekeza Irungu, ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji mkono wake wa kushoto, apelekwe kwenye Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.
Miongoni mwa watu ambao walifika mahakamani kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na Maribe, mbali ya wazazi wake walikuwa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na mkurugenzi wa zamani wa PSCU Dennis Itumbi.
Jaji Wakiaga, hata hivyo, alionya waandishi wa habari dhidi ya kutoa taarifa ambazo hazijawasilishwa mahakamani.