Maribe, Irungu wakana kumuua Monica Kimani

Muktasari:

  • Hata hivyo, watuhumiwa wawili hao watakaa mahabusu kwa siku nyingine mbili baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Jessy Lesiit kuamuru warejeshwe kortini hapo Jumatano ya Oktoba 17

Nairobi, Kenya. Mtangazaji maarufu wa Televisheni ya Citizen Jacque Maribe na mpenzi wake Joseph Irungu maarufu kama Jowie leo wamekana kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara mwanamke Monica Kimani.
Hata hivyo, watuhumiwa wawili hao watakaa mahabusu kwa siku nyingine mbili baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Jessy Lesiit kuamuru warejeshwe kortini hapo Jumatano ya Oktoba 17, siku ambayo itapangwa tarehe ya kusikiliza maombi ya dhamana yao.
Wakili wa Maribe, Katwa Kigen, alikuwa ameiomba mahakama kuharakisha tarehe za kutaja kesi kwa hoja kwamba washukiwa wamekuwa mahabusu kwa muda mrefu.
Irungu, mshukiwa mkuu katika kesi hiyo, alikamatwa Septemba 24 wakati mpenzi wake alinaswa siku tano baadaye.
Kimani aliuawa usiku wa Septemba 19, saa chache baada ya kuwasili Nairobi akitokea Sudan Kusini.
Mtuhumiwa wa tatu katika kesi hiyo Brian Kassaine, aliachiwa na mahakama wiki iliyopita lakini aliamriwa kuripoti mara kwa mara polisi.