Mtanzania afungwa Ghana kwa dawa za kulevya

Muktasari:

Taarifa kutoka Accra zinasema Mtanzania huyo alihukumiwa baada ya kukiri kosa la kusafirisha dawa  hizo za kulevya.

Dar es Salaam. Matukio ya watanzania kukamatwa na dawa za kulevya yameendelea kutawala baada ya Mtanzania mwingine ajulikanaye kwa jina la Basaida Zena Jafary kuhukumiwa miaka mitano  nchini Ghana baada ya kupatikana na gramu 300 ya dawa za kulevya.
Taarifa kutoka Accra zinasema Mtanzania huyo alihukumiwa baada ya kukiri kosa la kusafirisha dawa  hizo za kulevya.
Mtanzania huyo alikamatwa na maofisa wa bodi ya kupambana na dawa za kulevya nchini Ghana (Nacob) kwenye uwanja wa ndege wa ndege wa kimataifa wa Kotoka(KIA) wiki mbili zilizopita akiwa na kilo mbili na gramu 300 za Heroine na Cocaine.
Taarifa zilizotolewa na bodi hiyo na kunukuliwa na redio ya Star FM Online ya mjini Accra zimesema dawa hizo zilikuwa na thamani ya dola 70,000 (Sh 170Milioni) ambapo mtanzania huyo alikuwa akiwasili nchini humo ndege ya shirika la ndege la Rwanda yenye namba ET 200.
Taarifa hizo zinasema kwamba baada ya kukamatwa alifanyiwa upekuzi kwenye mzigo  ikabainika kwamba alikuwa amebeba dawa za kulevya.
Baada ya kugundilika kuwa ni dawa za kulevya, maofisa wa bodi hiyo walipelekwa mamlaka ya viwango kwa ajili ya uthibitisho ambayo pia ilibaini kwamba mzigo ule ulikuwa ni dawa.
Alipohojiwa alithibitisha kuwa ndiye mmiliki wa mzigo huo na alipewa na mtu anayejulikana kama Mwandenje Omari aishie Tanzania ambaye alimuagiza kuufikisha nchini Ghana kwa malipo ambayo hayakufahamika.