Friday, September 14, 2018

Mtatiro hakuishutumu Chadema

 

Dar es Salaam. Katika taarifa iliyochapishwa Alhamisi ya Septemba 13 na mtandao wa Mwananchi ilimnukuu mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro akitoa shutuma mbalimbali dhidi ya Chadema.

Mtatiro, ambaye sasa ni mwanachama wa CCM alikuwa katika kampeni za ubunge wa Jimbo la Ukonga eneo la Msongola na alizungumza na wananchi kwa dakika chache. Baada ya kupitia kwa makini malalamiko yake, tumejiridhisha kuwa mwandishi aliwachanganya wasemaji katika mkutano huo na Mtatiro hakutoa shutuma yoyote kwa Chadema.

Maneno yaliyomnukuu Mtatiro kimakosa yalizungumzwa na mtu anayeitwa Deo Mecky aliyedai mkutanoni hapo kuwa amewahi kuwa  msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Katika mkutano huo Mtatiro alizungumza kwa kifupi na alianza kwa kujitambulisha, “Majina yangu naitwa Julius Mtatiro, nimekuwa mkurugenzi wa kitaifa wa Chama cha Wananchi (CUF), nimekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara (Tanzania Bara) kwa miaka minne, nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa nikifanya majukumu ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa kwa miaka miwili, nimekuwa Katibu wa Ukawa katika Bunge Maalumu la Katiba na mwezi uliopita wakati naondoka na kuachana na Chama cha Wananchi CUF na kujiunga CCM nilikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Kidumu Chama cha Mapinduzi!”

Mtatiro aliendelea “...Kwa bahati mbaya nilichelewa, sikupata muda wa kuzungumza na muda umekwenda tumemuachia mgombea aweze kuendelea, nachotaka tu kusisitiza kwa wana Msongola na wana Ukonga ni kwamba tuko hapa kumsapoti Mwita Waitara, ukiona kiongozi kama mimi mkubwa kabisa kutoka chama cha upinzani ambaye amekaa miaka 10, baadaye ameachana na utapeli wa huko na amerudi Chama cha Mapinduzi, wewe kijana, mwanamama, kijana shtuka; Jumapili nenda kapige kura kwa Waitara. Kidumu Chama cha Mapinduzi!”

Kutokana na kosa hilo hatuna budi kumuomba radhi Mtatiro na wasomaji wetu.

Tayari tumechukua hatua za ndani – Mhariri

-->