Mtifuano wa viti maalumu CCM 2020

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa 2020, huenda ukaibua mtifuano ndani ya CCM, baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kusema upatikanaji wa wabunge wa viti maalumu kupitia jumuiya zake utaangaliwa upya.

Alisema mgawanyo wa wabunge wa viti hivyo kwa jumuiya zote tatu za CCM ambazo ni Wazazi, Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), unapaswa kuwa sawasawa.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi uliofanyika mjini Dodoma jana.

Kabla ya Rais Magufuli kutoa ahadi hiyo, mwenyekiti wa Wazazi anayemaliza muda wake, Abdallah Bulembo alimwomba kuwakumbuka wanachama wa jumuiya hiyo katika nafasi za uteuzi, akihoji uhaba wa wabunge wa viti maalumu ikilinganishwa na UWT na UVCCM.

“Ningeomba ombi hili katibu akushawishi utukubalie. Kwenye kipindi cha Rais aliyeondoka (Jakaya Kikwete), Jumuiya ya Wazazi ilikuwa haijawahi kuwa na wabunge wanawake, katika kipindi hicho tulipata wabunge wanawake wawili, nafasi za wanawake ndani ya CCM siyo za UWT,” alisema Bulembo.

“Ombi letu kwako, hatutaki kulingana na UWT, lakini Umoja wa Vijana wana nafasi kama nane, Wazazi wana dhambi gani leo kupewa wanawake wakawa wanane? Tunao wasomi wa kutosha.”

Ombi hilo lilipokewa kwa shangwe na wajumbe wa mkutano huo, lakini furaha yao ilizidi wakati mwenyekiti wa CCM aliposimama na kulijibu.

Katika sehemu ya hotuba yake, Rais Magufuli aliyetumia muda mwingi kuwasihi kuchagua viongozi wasiotumia rushwa, aliahidi kugawanya nafasi hizo ‘pasu kwa pasu’ akisema ni kutokana na mchango alioupata kutoka jumuiya hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Baada ya kuteuliwa majina, mlibaki na msimamo hata jumuiya nyingine mnafahamu zilivyoendelea kubebwa na kutokusimama imara. Kwa hiyo hili ombi la mwenyekiti la kuongezewa wabunge, kwamba kama UVCCM wanaingia watano kwa nini Jumuiya ya Wazazi aingie mmoja? Hii nitaifuta na tutaenda pasu kwa pasu,” alisema.

Katika utekelezaji wa ahadi hiyo, Rais Magufuli alisema ataangalia taratibu zinazotumiwa na jumuiya zote tatu kwa lengo la kuhakikisha zinakuwa sawasawa.

Kwa kauli hiyo, mabadiliko hayo huenda UWT ikapunguziwa idadi ya viti vya nafasi za uwakilishi ndani ya Bunge.

Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge, nafasi za wabunge wa viti maalumu ni 113, lakini 66 kati ya hizo ni wabunge kutoka CCM. Katika idadi hiyo ya CCM, UWT ina wabunge 58, UVCCM sita na Jumuiya ya Wazazi wawili.

Kwa hatua hiyo, mchuano wa kuwania viti maalumu katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia UWT utakuwa mkali kulinganisha na miaka ya nyuma.

Aliwaahidi wajumbe hao kuwa kwa kutumia nafasi yake ya uenyekiti atahakikisha nafasi hizo zinakuwa sawa.

Mbali ya ahadi hiyo, aliwahakikishia kuwa jumuiya hiyo haitafutwa katika uongozi wake akisema ilianzishwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alifahamu sababu za kuanzishwa kwake. “Nitakosa busara na nitalaaniwa ikiwa siku moja jumuiya hii itapotea kwenye mikono yangu.”

Pia, Rais Magufuli alisema hajafanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kutoka katika jumuiya hiyo kutokana na udhaifu katika uongozi wake.

Aliufananisha udhaifu huo na ule wa UWT ambao alisema ulikuwa umezidi. Alisema UWT haikuwa kwa manufaa ya wanachama bali kwa masilahi binafsi ya viongozi.

“Chagueni mkitanguliza dhamira zenu, najua mtazungumza kwamba wengine sikuwateua jumuiya ya wazazi, haikuwa hivyo hivyo kwenye Jumuiya ya UWT na UWT ilikuwa ni tatizo zaidi,kwa sababu orodha ya hata waliogombea au hata ambao wangependekezwa niwateue haikuletwa, kwa hiyo ni vigumu kujua CV (wasifu) ni ya nani, umteue nani aende wapi, ana uwezo gani, hilo ndilo lilikuwa tatizo. Kwa sababu viongozi hawakuwa na lengo la kusaidia UWT ila kusaidia maisha yao, kwa sababu waliwekwa na watu,” alisema Magufuli.

Awali, alimsifu Bulembo akisema uongozi wake unaiacha jumuiya hiyo ikiwa imepunguza asilimia 65 ya deni la Sh 4.8 bilioni walilokuwa wanadaiwa na kuongeza idadi ya wanachama.

Alisema alipoingia madarakani uongozi uliorodhesha mali zote za chama, kufanya tathmini na kuimarisha usimamizi.

Alisema baada ya kazi hiyo, hatimiliki ziliongezeka kutoka 18 hadi kufikia 54, idadi ya wanachama ilifikia 861,795, wanachama wote kuwa na bima ya afya, kuboresha shule za jumuiya hiyo huku uongozi huo ukiacha mapato ya Sh2.1bilioni.