Mtikisiko Acacia

Muktasari:

Acacia ni kampuni tanzu ya Barrick Gold inayomiliki migodi mitatu ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara. Ilizuiwa kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje tangu Machi, lakini mazungumzo kati ya Serikali na Barrick, yamezaa makubaliano ambayo pia yanaitaka Acacia kulipa dola 300 milioni za Marekani.

Dar es Salaam. Wiki mbili baada ya Serikali na Barrick Gold kufikia makubaliano kuhusu biashara ya dhahabu, kampuni tanzu ya Acacia imetangaza kujiuzulu kwa maofisa wake wawili wa ngazi za juu.

Acacia ni kampuni tanzu ya Barrick Gold inayomiliki migodi mitatu ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara. Ilizuiwa kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje tangu Machi, lakini mazungumzo kati ya Serikali na Barrick, yamezaa makubaliano ambayo pia yanaitaka Acacia kulipa dola 300 milioni za Marekani.

Kuna habari kuwa Serikali ilikataa kufanya mazungumzo na Acacia kuhusu usafirishaji wa mchanga wa madini uliozuiwa bandarini kwa ajili ya uchunguzi na muda wote imekuwa ikifanya mazungumzo na John Thorntorn, mwenyekiti mtendaji wa Barrick Gold, inayomiliki asilimia 64 ya hisa za Acacia.

Wakati utekelezaji wa makubaliano hayo yaliyopingwa na Acacia haujaanza, kampuni hiyo ya Canada jana ilitangaza kuwa ofisa mtendaji wake mkuu, Brad Gordon amejiuzulu ili aweze kurudi nyumbani kwake Australia kusimamia masuala ya familia yake, wakati ofisa mkuu wa fedha, Andrew Wray amepata fursa nzuri zaidi sehemu nyingine.

Mwenyekiti wa bodi ya Acacia, Kelvin Dushnisky amewashukuru wawili hao, akisema walikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya kampuni hiyo ndani ya miaka minne iliyopita na kuwatakia kila la heri waendako.

“Brad na Andrew wamekuwa muhimu katika mafanikio ya Acacia katika uendeshaji na faida katika kipindi cha miaka minne na kwa niaba ya bodi na kampuni, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote wawili kwa mchango wao,” alisema Dushnisky.

“Tunaimani Peter (Geleta) na Jaco (Meritz) watatekeleza majukumu yao mapya kwa kiwango hicho. Bodi itaendelea kutoa ushirikiano kwa menejimenti wakati kampuni ikijikita katika kuhakikisha inafikia malengo yetu ya uendeshaji, ambayo yatabakia vilevile kama ilivyokuwa katika robo ya tatu, huku tukiendelea kutafuta muafaka na Serikali ya Tanzania.”

Kuziba nafasi za wawili hao, bodi ya Acacia imemtangaza Peter Geleta kuchukua majukumu ya ofisa mtendaji mkuu badala ya Gordon, na Jaco Maritz kusimamia masuala ya fedha za kampuni hiyo.

Wote wawili walikuwa watendaji wa Acacia kwa muda mrefu. Geleta alikuwa mkuu wa oganaizesheni wakati Maritz alikuwa meneja mkuu wa idara ya fedha.

Pamoja na uamuzi huo wa kujiondoa kwenye operesheni za kampuni, taarifa ya Acacia iliyotolewa jana asubuhi inasema wote wawili, Gordon na Wray wataendelea na majukumu yao hadi mwishoni mwa mwaka watakapokabidhi ofisi kwa warithi wao.

“Licha ya majukumu ya uendeshaji, Geleta atahudhuria vikao vya bodi vitakavyofanyika mwishoni mwa mwaka huu badala ya Gordon na kuifanya idadi ya wajumbe kuendelea kubaki saba,” inasema taarifa hiyo.

Kwa miezi miwili iliyobaki, makabidhiano ya ofisi yataendelea kufanyika mpaka Januari Mosi, mwakani yatakapohitimishwa na uongozi mpya kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza na tovuti ya Fiancial Times baada ya taarifa hizo, Richard Hatch, mchambuzi katika soko la hisa la RBC, alisema uamuzi huo si wa kustua, lakini una athari.

“Kwa mazingira ya changamoto yaliyopo Tanzania, na nafasi ndogo ya menejimenti kushiriki katika mazungumzo na Serikali, tunaamini tangazo hili si la kustua katika soko,” alisema Hatch.

“Hata hivyo, tunaangalia kuondoka kwa Gordon na Wray kuwa na mtazamo hasi katika hisa za Acacia, hasa kutokana na mafanikio waliyopata katika biashara tangu wateuliwe kushika nafasi zao, kwa kuangalia uendeshaji na faida.”

Ndani ya wiki mbili baada ya majadiliano ya Serikali na Barrick Gold, uongozi wa Acacia ulikuwa na msimamo tofauti, ukisema hauna fedha za kulipa kwa mkupuo dola 300 milioni zilizoahidiwa na Thorntorn katika mazungumzo na Serikali, akisema ni kwa ajili ya kuonyesha “nia njema”.

Wakati Acacia ilipotangaza taarifa yake ya fedha ya robo ya tatu Oktoba 20, Wray aliwaambia waandishi wa habari kuwa kampuni hiyo haina uwezo wa kulipa kiasi hicho kwa mkupuo.

Kwa kipindi hicho, faida ya Acacia imepungua kutoka Dola 52.7 milioni za mwaka jana mpaka Dola 16 milioni katika miezi mitatu kuanzia Julai mpaka Septemba. Hata hivyo, kwa miezi tisa mfululizo, faida hiyo imeongezeka kutoka dola 48.4 milioni mpaka dola 78.5 milioni.

Kwenye taarifa hizo, Acacia imetenga dola 128 milioni kwa ajili ya malipo ya kodi huku Barrick ikiandaa Dola 172 milioni zitakazokamilisha malipo ya jumla ya dola 300 milioni zilizoafikiwa.

Wachambuzi

Baadhi ya wachambuzi wanaamini msimamo wa kutokubali kutekeleza makubaliano baina ya Barrick na Serikali ndicho kilichowashawishi viongozi hao kuachia ngazi.

Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema si kwamba Gordon na mwenzake wamejiuzulu, bali wameondolewa kutokana na msimamo wao usiokubalika kwa Barrick na Serikali na kwamba kuondoka kwao kutafanikisha utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa.

“Nawapongeza Acacia kwa kumuondoa Gordon na kumweka Geleta ambaye ana ushirikiano mzuri na jamii jirani. Gordon ana msimamo wa kinyonyaji na kwa kushirikiana na Wray hawakuwa tayari kutekeleza kilichoafikiwa. Waliorithi nafasi zao wamejifunza hili,” alisema Maige.

Alipongeza njia aliyoitumia Rais John Magufuli kuwabana wachimbaji hao wakubwa wa dhahabu nchini kiasi cha kuwashawishi Barrick kuja kufanya mazungumzo.

“Acacia ni jeuri ndio maana hata baada ya majadiliano wameendeleza ukaidi katika kutekeleza kilichoafikiwa. Kwa muda mrefu nimekuwa nikilalamikia uhusiano usioridhisha kati ya kampuni hiyo na wananchi wanaozunguka migodi yao. Hawakuwa wanatusikiliza. Natarajia kutakuwa na mabadiliko,” alisema mbunge huyo.

Wapo wanaoamini kwamba kila inapojitokeza changamoto kubwa, viongozi wa juu wanapaswa kuenguliwa ili kuendelea kujenga imani mbele ya wadau.

Mhadhiri mwandamizi wa biashara na menejimenti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Dianna Mwiru alisema sababu zilizotolewa na watendaji hao wa juu wa Acacia huenda zikawa sahihi au ni kificho.

Alisema kwa udanganyifu uliobainika chini ya uongozi wao, kunapunguza kuaminika kwao ndani na nje ya wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba kwa mwekezaji yeyote lazima angewachukulia hatua.

“Hata ningekuwa mimi ndiye mmiliki wa Acacia na nimegundua wamehusika kwenye udanganyifu huu, ningewataka waondoke,” alisema msomi huyo.

Licha ya sababu za kung’atuka kwa viongozi hao, Dk Mwiru alisema huenda wamechangia Acacia kukiuka mkataba baina yake na Serikali, hasa kwenye biashara ya makinikia kutokana na nafasi zao.