Mtindo wa maisha waibua saratani kivingine

Wagonjwa mbalimbali wa saratani wakiwa wamelazwa katika wodi wakipatiwa tiba ya kemikali kwa dripu ‘Chemotherapy’, kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Ugonjwa huo ambao mara nyingi ilielezwa unasababishwa na mtindo wa maisha na aina fulani ya vyakula, wataalamu wanasema hivi sasa asilimia 60 ya wagonjwa wapya wamesababishiwa ugonjwa huo na vijidudu.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa ugonjwa wa saratani uliodhaniwa kuwaathiri zaidi wazee na watu wa mataifa makubwa, umeibuka kwa sura mpya na kasi nchini, ukiathiri zaidi tumbo, koo na kinywa.

Ugonjwa huo ambao mara nyingi ilielezwa unasababishwa na mtindo wa maisha na aina fulani ya vyakula, wataalamu wanasema hivi sasa asilimia 60 ya wagonjwa wapya wamesababishiwa ugonjwa huo na vijidudu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa ORCI, Crispin Kahesa amesema licha ya ongezeko la wagonjwa, aina nyingi za saratani zimesababishwa na virusi, bakteria na visababishi vingine kama kichocho.

“Kwa mfano saratani ya shingo ya kizazi inasababishwa na virusi vya Human Papiloma Virus (HPV) ambayo vinasambazwa kwa njia ya ngono, saratani ya kibofu cha mkojo kinasabishwa na kichocho, saratani ya tumbo inasababishwa na ‘helicobakter pylori’ ambazo ni bacteria, saratani ya ngozi inasababishwa na HHV 8 ambavyo ni virusi,” amesema Dk Kahesa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage alisema taasisi hiyo inahudumia wagonjwa wa tiba ya kemikali ‘Chemotherapy’ kati ya 50 hadi 70 kwa siku, huku ikilaza wagonjwa zaidi ya 259.