Mtolea wa CUF aliamsha dude la mafuta, sukari

Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea

Dodoma. Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea ameitaka Serikali kuwaeleza Watanzania ni lini bei ya sukari na mafuta ya kula itapungua kama walivyoahidiwa.

 

Akichangia Bajeti ya Serikali na taarifa ya hali ya uchumi leo Juni 21, 2018 bungeni mjini Dodoma, Mtolea amesema kipimo cha pato la Mtanzania kinapaswa kupimwa kwa kumwezesha kupata milo mitatu.

 

“Mwaka 2015 kilo ya sukari ilikuwa Sh1,200, lakini mwaka 2017 ikafika Sh2,500, mkalieleza Bunge na Taifa kwamba ni hujuma ya wafanyabishara kwamba imefichwa katika maghala, lakini hamjaja hapa kuwaeleza tena Watanzania, lakini leo hii kilo ya sukari imefika Sh3,000 sasa tunajiuliza hiyo bei mnayoidhibiti ni ipi,” amehoji Mtolea.

 

“Lilitokea tatizo la mafuta ya kula, Waziri Mkuu akatoa siku tatu hapa bungeni wenye mafuta wayatoe baada ya bei kuwa juu na kuadimika, mpaka leo hatujaelezwa hapa bei kwa nini iko juu. Sasa huu mfumuko wa bei mnaosema mnaudhibiti ni upi na lini bei itapungua.”

 

Mtolea amesema inashangaza kuona viongozi wanapanda majukwaani na kujisifu kununua Bombadier na kujenga Stieglers Gorge, badala ya kujisifu kwamba wamemwezesha mwananchi kula milo mitatu.

 

Bajeti ya Serikali inaendelea kujadiliwa na wabunge tangu ilipowasilishwa Alhamisi wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.