Mtoto aliyetekwa azidi kuibua machungu, akosa vipindi 56 shuleni

Mtoto aliyetekwa Idrissa Ally

Muktasari:

Mwalimu mkuu amzungumzia kwa hisia nzito, mzazi awaangukia Watanzania, polisi kuokoa maisha ya mwanaye

Dar es Salaam. Mussa Idrissa, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Princes Gate anayosoma mtoto aliyetekwa Idrissa Ally (13), amesema kutoweka kwa mwanafunzi huyo kumemfanya akose vipindi 56 vya masomo.

Idrissa, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo alitekwa Septemba 26 saa 11 jioni akicheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva wa kiume aliyekuwa na gari aina ya Toyota IST ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa kuwa ni sumu na kumpulizia kisha kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake na kutoweka naye.

Akizungumza jana na Mwananchi, mwalimu huyo alisema vipindi hivyo ni kwa siku nane ambazo mwanafunzi huyo hajahudhuria darasani tangu alipotoweka.

“Darasa la Idrissa kwa siku wanasoma vipindi saba, ukizidisha mara nane ambazo hayupo darasani unapata 56. Vipindi hivi ni vile ambavyo sasa hivi wanafunzi wenzake wanafanya revision (marudio) ya baadhi ya mada za masomo waliyoyasoma miezi iliyopita,” alisema Mwalimu Idrissa.

Alisema  wanafunzi  na walimu wanaomfundisha wanajisikia vibaya kutomuona mwanafunzi huyo ambaye jana alitimiza siku 13 baada ya kutekwa maeneo ya nyumbani kwao.

“Watanzania watusaidie, hilo janga siyo la Idrissa pekee ni watu wote. Tushirikiane kuhakikisha linatokomezwa na kutoa taarifa zitakazosaidia upatikanaji watoto waliokumbwa na matatizo kama haya akiwamo Idrissa,” alisema.

Aliongeza kuwa, “endapo Idrissa akipatikana litakuwa jambo la heri ingawa hataweza kufanya vizuri mitihani ya mwisho wa mwaka kwa sababu maandalizi yake yatakuwa ni hafifu.”

Juzi,  Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema  bado wanaendelea kumtafuta mwanafunzi huyo.

“Bado hatujampata Idrissa, upelelezi wa kumtafuta unaendelea  tukishirikiana na wazazi wake,” alisema Mambosasa kwa ufupi.

Baba mzazi wa Idrissa, Ally Idd alisema bado mwanaye hajapatikana lakini  wanaendelea na juhudi za kumtafuta wakishirikiana na polisi.

“Ingawa familia inaendelea kuhangaika kumtafuta Idrissa, lakini jukumu kubwa tumewaachia polisi kutokana na uwezo wao,” alisema mzazi huyo.

Idd alitumia nafasi kutoa wito kwa Watanzania popote watakapomuona mtoto wake watoe taarifa polisi.

Septemba 23, mtoto Beauty Yohana (3) aliibwa katika Kanisa la FPCT Mbezi Mwisho na kupatikana baada ya saa 48.

Alipatikana maeneo ya Kivule akiwa na msichana Angel Vincent (19).