Mtoto auawa, mwili wafungwa kwenye kiroba

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley

Muktasari:

  • Mtoto Aisha Husseni (4) ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha juzi Septemba 22, 2018 mkoani Tabora, ameokotwa katika shamba la migomba  akiwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa umefungwa kwenye kiroba

Tabora. Mtoto  Aisha Husseni (4) ameokotwa akiwa kwenye mfuko wa sandarusi akiwa amechomwa moto na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea mtaa wa Sukuma jana Septemba 23, 2018 katika kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema tukio hilo limetokea na uchunguzi unaendelea kufahamu nini kimetokea kwa mtoto huyo na wahusika kubainika.

Baba mzazi wa mtoto huyo Hussein Maulid amesema walianza kumtafuta mtoto wao kuanzia juzi pasipo mafanikio na asubuhi ya jana walielezwa wameuona mwili wa mwanaye ukiwa kwenye migomba.

“Tulimtafuta kila mahali na hatimaye kutoa taarifa kwa watu na kwenye msikiti kutangaziwa wananchi kuhusu kupotea kwake,” amesema.

Shangazi wa marehemu Amina Maulid, amesema baadhi ya watu waliuona mwili ukiwa umezingirwa kwenye mfuko wa sandarusi ukiwa umeunguzwa baadhi ya sehemu.

Diwani wa Mbugani, Paul Kananda amesema ni tukio la kikatili ambalo haliwezi kufumbiwa macho na kutaka vyombo vya dola kuwabaini wahusika wa mauaji ya mtoto huyo.

“Huyu ni mtoto mdogo watu wamemuunguza kuanzia kiunoni kwenda miguuni kama angekuwa mkubwa tungedhani mengine lakini huu ni ukatili,” amesema.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sukuma, Abdallah Salim amesema mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na kukutwa ameuawa.

Alivitaka vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wote wanatafutwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa vile kitendo hicho hakikubaliki.

Hilo ni tukio la kwanza kutokea kwa mtoto kuuawa na kuchomwa moto katika kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora.