Mtoto wa miaka miwili ajipiga risasi hadi kufa

Muktasari:

Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya watoto kujipiga risasi nchini Marekani

Texas, Marekani. Polisi katika Jimbo la Texas nchini Marekani imesema inachunguza tukio la mtoto wa umri wa miaka miwili kujipiga risasi kichwani kwa bunduki ambayo imekuwa ikihifadhiwa na wazazi wake nyumbani kwao. Mtoto huyo amefariki dunia.

Wakati wa tukio hilo, wazazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Christopher Williams Jr walikuwa nyumbani. Polisi wanasema bunduki hiyo ilikuwa inamilikiwa na baba yake.

Hata sasa bado haijafahamika mara moja kama wazazi wa mtoto huyo watashtakiwa. Watoto kadhaa wamekuwa wakijipiga risasi na kujiua kimakosa nchini Marekani katika miaka ya karibuni.

Polisi mjini Houston wamesema wanajaribu kubaini ni vipi mtoto huyo aliweza kuifikia bunduki hiyo.

Mkuu wa kitengo cha waathiriwa maalum katika idara ya polisi ya Houston, David Angelo ametoa wito kwa wazazi walio na bunduki kuchukua tahadhari zaidi.

“Ni lazima uweke salama silaha, iwe ni kwa kuhakikisha kifaa cha kufyatulia risasi kimewekwa salama au kuiweka salama silaha kwa njia nyingine kuhakikisha matukio kama haya hayatokei tena siku za usoni,” alisema.

Mapema wiki hii polisi katika mji wa Houston walimshtaki baba mwingine kutokana na kujipiga risasi kimakosa kwa mwanawe wa kiume. Mtoto huyo alikumbwa na mkasa huo Mei mwaka huu.

Ali Parvez Masoom anadaiwa kuiacha bunduki yake mezani ambapo mwanawe aliweza kuifikia na kujipiga risasi usoni.

Masoom aliachiwa huru baada ya kulipa dhamana ya Dola 1,000 na kwa sasa anakabiliwa na kosa la kutowajibika na kumuwezesha mtoto kuifikia silaha.

Wiki iliyopita mtoto mwingine wa miaka miwili alifariki dunia California katika kisa kinachotajwa kukaribiana na hicho. Wazazi wa mtoto huyo walikuwa nyumbani alipoifikia bastola hiyo na kujipiga risasi kichwani.

Machi 19, mvulana wa miaka tisa nchini humo alidaiwa kumuua dadake wa miaka 13 kwa kumpiga risasi kichwani baada ya mzozo kuhusu kifaa cha kudhibiti mchezo wa video wa kompyuta.

Mvulana huyo kutoka Jimbo la Mississippi anadaiwa kuchukua bunduki baada ya dada yake kukataa kumpa kifaa hicho.

Alimpiga risasi kichwani kutoka kisogoni na risasi hiyo ikaingia hadi kwenye ubongo.

Haijabainika ni vipi mvulana huyo alipata bunduki hiyo na pia bado haijabainika ni hatua gani zitachukuliwa dhidi yake.

“Ni mtoto wa miaka tisa tu,” mkuu wa wa tarafa ya Monroe Cecil Cantrell aliliambia gazeti la Clarion Ledger na kuongeza:

“Nafikiria kwamba ametazama hili kwenye michezo ya video ya kompyuta au kwenye runinga. Sijui iwapo alifahamu hasa nini alichokuwa anakifanya. Siwezi kujibu hilo. Najua tu kwamba ni mkasa, kisa cha kusikitisha.”

Mama ya watoto hao alikuwa kwenye chumba kingine, akiwalisha watoto wengine kisa hicho kilipotokea.

Polisi walianzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho, ikiwa ni pamoja na jinsi mtoto huyo alivyoweza kuifikia bastola hiyo.

“Hili ni jambo geni sana kwetu, hatujawahi kukumbana na mtoto wa miaka tisa aliyempiga risasi mtoto mwenzake,” mkuu huyo aliwaambia waandishi wa habari.