Mtu mrefu hajapata matibabu

Baraka Elias

Muktasari:

  • Elias, anayesumbuliwa na matatizo ya nyonga alitakiwa kupelekwa nchini India kwa matibabu.
  • Kijana huyo alipata matatizo ya nyonga Aprili mwaka jana, baada ya kuanguka nyumbani kwao mkoani Ruvuma, alikuja jijini Dar es Salaam kwa matibabu lakini  alielezwa kuwa kutokana na ukubwa wa mwili na urefu wake, baadhi ya vipimo vinakosekana hivyo kutakiwa kwenda nje kwa matibabu zaidi.

Dar es Salaam. Baraka Elias, mtu mwenye urefu wa futi 7.4 aliyeahidiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu Januari 22 baada ya kupewa rufaa na Taasisi ya Mifupa (Moi), hadi sasa hajui hatima yake kutokana na ukimya wa Wizara ya Wizara ya Afya.

Elias, anayesumbuliwa na matatizo ya nyonga alitakiwa kupelekwa nchini India kwa matibabu.

Kijana huyo alipata matatizo ya nyonga Aprili mwaka jana, baada ya kuanguka nyumbani kwao mkoani Ruvuma, alikuja jijini Dar es Salaam kwa matibabu lakini  alielezwa kuwa kutokana na ukubwa wa mwili na urefu wake, baadhi ya vipimo vinakosekana hivyo kutakiwa kwenda nje kwa matibabu zaidi.

Elias aliiambia Mwananchi jana kuwa, hafahamu chochote kinachoendelea kuhusu matibabu yake zaidi ya kuendelea kuteseka kwa maumivu na amekuwa akifuatilia mara kwa mara suala hilo.

 Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja alisema  Elias anatakiwa kufika wizarani kuulizia hatma ya safari yake wakati wowote anapoona inafaa kufanya hivyo.

“Taratibu kuhusu safari yake zinaandaliwa. Katika orodha yetu kuna wagonjwa wengi ambao wanasubiri, kwa suala lake lilipofikia tunashughulikia usafiri. Nashauri kesho (leo) afike wizarani kujua kinaendelea,” alisema Mwamaja.