Mtulia awashukuru waliompigia kura

Muktasari:

Mtulia azungumzia idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza.


Dar es Salaam. Mshindi wa ubunge jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia amewashukuru wananchi na hasa waliojitokeza kumpigia kura wakiamini atawaletea maendeleo.

Mtulia ametangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika jana Februari 17,2018.

Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli ametangaza matokeo hayo leo Februari 18,2018.

Katika uchaguzi huo Mtulia amepata kura 30,247 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu aliyepata kura 12,353; huku Rajab Salum Juma wa CUF akipata kura 1,943.

Amesema idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa 264,055 lakini waliojitokeza walikuwa 45,454.

Kagurumjuli amesema kura halali zilikuwa 44,867 na zilizokataliwa zilikuwa 587. Uchaguzi ulihusisha wagombea 12.

Wagombea wa vyama vingine walioshiriki uchaguzi huo na idadi ya kura walizopata katika mabano ni; Ally Omari Abdallah wa Ada Tadea (97), Bashiri Kiwendu wa AFP (12), George Kristian wa CCK (129), Mary Mpangala wa DP (21), John Mboya wa Demokrasia Makini (10), Mohamed Majaliwa Mohamed wa NRA (15), Johnson Mwangosi wa SAU (11), Godfrey Malisa wa TLP (14) na Mwajuma Milambo wa UMD (15).

Mtulia akizungumzia kuhusu watu wachache kujitokeza kupiga kura, amesema ni kwa sababu hapakuwa na mgombea wa udiwani.

“Mwitikio huu umetokana na kuwa ni uchaguzi mdogo, wapo pia wanaoamini hata wakimchagua mbunge haendi kufanya kitu chochote, lakini hawa walionichagua wamewawakilisha wenzao, nitakwenda kufanya kazi nao bila kujali ni wa chama gani,” amesema.

Mtulia amewashukuru wadau wa usalama kwa juhudi za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Pia, ameishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa namna ilivyofanikisha uchaguzi huo akisema anaamini kila mmoja atakuwa ameridhika kwamba uchaguzi ulikuwa huru na haki.

“Kushindwa ni kawaida na ilikuwa lazima apatikane mshindi,” ameshinda.

Amesema anawashukuru waandishi wa habari kwa kufikisha sera, vipaumbele na dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kinondoni.

“Shukrani kwa wagombea wenzangu 12, hii ni dalili kuwa nchi imekomaa kidemokrasia,” amesema.

Amesema wapo waliofanya kampeni za nyumba kwa nyumba na mihadhara; kila mmoja kwa namna alivyoona inafaa.

“Si mkongwe sana kwenye chama nimeingia Desemba 4,2017 chama kikanipa ridhaa na nafasi ya kupeperusha bendera,” amesema Mtulia aliyekuwa mbunge jimboni humo kwa tiketi ya CUF kabla ya kujiuzulu na kujiunga na CCM.

Amewashukuru wanachama wa CCM, na hasa Idd Azzan na Abbas Tarimba waliowahi kuwa wabunge wa Kinondoni.

“Ninachowaahidi nitashirikiana nanyi kwa sababu matatizo ya Kinondoni ninayajua; kuboresha miundombinu, tatizo la ajira yote nitakwenda kuyafanyia kazi,” amesema.

Amesema anaamini wabunge wenzake watampa ushirikiano kwa kuwa amefanya nao kampeni na wameona matatizo ya Kinondoni ambayo hahitaji kuwaelezea.

Mgombea wa chama cha DP jimboni humo, Mary Mpangala amesema uchaguzi umekwenda vizuri na kwa haki.

Ameshauri katika uchaguzi mwingine wapiga kura wapewe elimu zaidi.

Mwajuma Milambo wa chama cha UMD aliyegombea ubunge jimboni humo amesema uchaguzi ulikuwa wa amani tofauti na mwanzo akisema walikuwa na hofu kwa kutojua utakuwaje.

“Kinondoni ndiyo Dar, kwa wadau wa siasa kulikuwa na sintofahamu nyingi, nashukuru wananchi wamejitokeza ingawa si kwa wingi ila wameonyesha nia ya kupata kiongozi wamtakaye,” amesema.