Mtulia ajutia ushindi mkubwa, Dk Mollel asema aliumiza wengi

Muktasari:

Wagombea hao walirejeshwa na chama hicho tawala kugombea ubunge katika majimbo hayo.

Dar/Kilimanjaro. Unaweza kusema uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo umeanza kwa staili ya aina yake baada ya mgombea wa jimbo la Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia kuwaomba radhi wanachama wa chama hicho tawala kwa ushindi wa kishindo alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 akiwa CUF.

Pia mgombea wa CCM wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Dk Godwin Mollel alisema uamuzi wake wa kujivua ubunge uliwaumiza wengi, lakini alisema umelenga kuwasaidia, huku Waziri wa Mambo ya Ndani akisema wapinzani wengi watajiunga CCM kwa sababu miiko ya vyama vingi imekiukwa.

Uchaguzi katika majimbo hayo unafanyika baada ya Mtulia na Dk Godwin Mollel aliyekuwa mbunge wa Siha (Chadema), wote kuhamia CCM, Desemba mwaka jana na hivyo kupoteza sifa za kuwa wabunge.

Wagombea hao walirejeshwa na chama hicho tawala kugombea ubunge katika majimbo hayo.

“Nawaomba msamaha kwa yote niliyowakwaza wakati wa kampeni na kushinda kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi 2015,” alisema Mtulia aliyeshinda ubunge kwa tiketi ya CUF na kuungwa mkono na Ukawa.

“Mnisamehe mtoto wenu nimerudi nyumbani kwenye chama kubwa. Niliwapa kadi lakini mmeamua kunipa ubunge.”

Mtulia alisema vyama vyote vya upinzani ni sawa na asasi za kiraia, kwamba ni tofauti na ilivyo CCM kwa madai kuwa wapinzani wanasaka pesa na si kusaidia wananchi.

Alitaja sababu iliyomfanya kuhama CUF kwamba ni baada ya kuona viongozi wake wakuu hawaelewani, huku akisisitiza kuwa nje ya CCM ni sawa na kujenga ukuta.

Mtulia aliambatana na wanachama wa CUF walioamua kujiunga na CCM na kukabidhiwa kadi.

Akizungumza katika utambulisho huo, mwenyekiti wa CCM wilayani Kinondoni, Haloid Maluma aliwataka wanachama kuwa na ushirikiano kukipa ushindi chama hicho.

“Mgombea wetu ni Mtulia. Naomba wenyeviti wa mashina, kata na matawi na jumuiya zake tuwe na ushirikiano,” alisema na kuiwataka kutunza siri za vikao.

“Tufanye kampeni na uchaguzi wa kisayansi. Kila mmoja wenu ajue ana wanachama wangapi katika eneo lake.”

Kwa upande wake Mwigulu alisema upinzani Afrika na Tanzania umekuwa wa kupinga kila kitu hata kama Serikali imefanya jambo jema.

“Kwa nchi za wenzetu Serikali ikifanya jambo jema wanasifia na kueleza namna ya kuliboresha zaidi, lakini kwetu upinzani ni kupinga kila kitu na kama ni mpinzani ukisifia, unaitwa kuhojiwa. Hii si sawa kabisa,” alisema.

“Twendeni tumuunge mkono Mollel akatekeleze ilani ya Serikali iliyoko madarakani kwa kuwa kwa sasa hatuinadi ilani bali mipango ya kutekeleza na kuwaletea maendeleo.”

Dk Mollel alisema alifanya uamuzi mgumu uliowaumiza wengi kwa kuwa ni ushujaa wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Siha.

Aliwaomba wananchi kumuunga mkono na kuhakikisha anapata tena nafasi hiyo ili kwenda kuungana na Rais John Magufuli.

Wakati wakuu wa wilaya, ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katioka maeneo yao, walilaumiwa kwa kuingilia uchaguzi wa madiwani, mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alihudhuria mkutano huo wa kampeni na kupata fursa ya kuzungumza.

Mbali na kuzungumzia suala la amani, Buswelu alimuombea kura Dk Mollel.

Alisema Serikali haijaribiwi, hivyo ni vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni.

Alisema Dk Mollel ameleta heshima kwa wananchi wa jimbo hilo na kuwataka wote kumuunga mkono na kuhakikisha anapata ushindi wa kishindo.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema safari ya kusaka ubunge imeanza na kuwataka wananchi kumuunga Dk Mollel.

Mgombea ubunge wa CUF jimbo la Kinondoni, Rajabu Salum Juma naye alizindua kampeni zake jana katika viwanja vya Ally Mapilau na kutaka wananchi wa wamchague ili awaletee maendeleo.

“Naomba mnichague mimi mzaliwa wa Kinondoni ninayejua changamoto zenu. Msidanganyike kumpa mgombea wa chadema wala CCM,” alisema Juma ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2015, alikuwa meneja wa kampeni wa Mtulia.

Alisema akichaguliwa atafanya maboresho katika soko la Kinondoni, atakutana na wananchi kukusanya kero zao ili kuziwasilisha bungeni kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Imeandikwa na Jackline Masinde, Pamela Chilongola (Dar) na Florah Temba (Kilimanjaro)