Mtulia akabidhiwa kadi CCM, CUF ikiwaomba radhi Kinondoni

Aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (aliyevaa miwani) akishangiliwa na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada kujiunga rasmi na chama hicho, jijini Dar es Salaam. Mtulia alijiuzulu ubunge baada ya kutangazo kujivua uwanachama wa CUF. Picha na Salim shao

Muktasari:

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya CCM, Mtulia alisema amehamia chama ambacho anaweza kuwatumikia wananchi kuliko alikokuwa.

       Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akikabidhiwa kadi ya CCM, chama chake cha zamani CUF kimewaomba radhi wapiga kura wa Jimbo la Kinondoni baada ya mwanachama huyo kujiuzulu nafasi hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya CCM, Mtulia alisema amehamia chama ambacho anaweza kuwatumikia wananchi kuliko alikokuwa.

Alisema Rais John Magufuli alipokuwa akizindua ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota alijitokeza na kuzungumza naye kuhusu maendeleo ya Kinondoni, jambo ambalo lilionekana ni kinyume na upinzani.

“Hili nalo lilileta shida na kuonekana sikufanya sawa, nimeona nije huku kabisa, kwa sababu ilikuwa ngumu kwangu kuwatumikia wananchi,” alisema.

“Kingine chama changu cha CUF kina migogoro isiyokwisha, hujui ukae upande upi, inakuwa ngumu kuwatumikia waliokuchagua katika utendaji wa namna hii nimeamua kuhama.”

Alisema kwa kuwa mbunge wa CUF ameshindwa kufanya mambo mengi, tofauti na angekuwa CCM.

“Msaada wangu kwa wananchi, utekelezaji wa majukumu yangu kwao nikiwa CUF ulikuwa mdogo, ninachowashauri uchaguzi ujao wasifanye makosa tena wamchague wa CCM ili aweze kutatua kero zao. ” alisema Mtulia.

Mtulia alisema anaamini hatajutia uamuzi wake na hajahamia huko kwa ajili ya kufuata vyeo, hivyo hata akiambiwa awe msaidizi wa mjumbe wa nyumba 10 yupo tayari. “Kama nafasi hiyo pia itakuwa imejaa sina shida nitarudi Rufiji kwenye asili yangu nikavue samaki,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Aroun Maluma ambaye alimkabidhi kadi ya uanachama wa CCM, alisema wanaotaka kuhamia kwenye chama hicho wanakaribishwa, lakini kwa kufuata taratibu.

Alisema hakuna mwanachama atakayekubaliwa bila kupitia katika ngazi za chini ajadiliwe na akionekana anafaa atakubaliwa.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tandale, Tamim Omary alisema ujio wa Mtulia ndani ya chama hicho utawavuta wengi kutoka CUF kwa sababu jahazi limetoboka na sasa maji yapo magotini.

Alisema mbali ya kuwapata wengi, pia watasikia mengi ikiwamo namna alivyoshinda ubunge wa jimbo hilo.

“Ana siri nyingi huyu, ataeleza hadi chochoro alizopita hadi kuwa mbunge wa Jimbo la Kinondoni, wanakuja wengi kutoka CUF tulieni tu, ”alisema.

CUF waomba radhi

Akiomba radhi kutokana na mbunge huyo kuhamia CCM, mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma wa CUF, Abdul Kambaya alisema walimsimamisha Mtulia kuwania nafasi hiyo na hatimaye wananchi wa Kinondoni wakampa kura wakiamini ni mtu makini, lakini bahati mbaya amewageuka.

“Mtulia amesahau tulikesha siku tatu tukishinikiza atangazwe kuwa mbunge, wapo waliopigwa, wenye kesi na wengine ni vilema kwa sababu ya kupigania haki yake,” alisema Kambaya.

Alisema wapo watu waliojengwa na matumaini kutokana na sera za CUF na wakamwamini kwa kumpa kura Mtulia, lakini aliyoyafanya siyo tu kuwadidimiza kisiasa, bali yataondoa uaminifu kwa vijana.

Kambaya alisema msimamo wa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ni kuwa hawajafurahishwa na uamuzi uliofanywa na Mtulia ambao upo tofauti na ule wa upande unaomuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif uliofurahia hatua hiyo.

“Wana-CUF wapo imara tutaingia Jimbo la Kinondoni na tutagombea tena na tutapambana kwa sababu hiki chama kina misingi, asili na waumini siyo wanachama tu na kitaendelea kuwepo,” alisema.

“Kama Maulid (Mtulia) anadhani ametukomoa sisi kutokana na nafsi yake atakuwa amejidanganya na ameishushia heshima familia yake. ”

Alifafanua kuwa kinachoonekana si mnunuaji bali tatizo ni muuzaji, kwa sababu mnunuaji atakosa muuzaji hakuna biashara na kilichopo kwa viongozi waliopata fursa ni wenyewe kuwa na viashiria vya kujiweka sokoni.

Alisema kwa wana-CUF wanaomjua Mtulia mwaka 2005 alishinda kura za maoni za kugombea udiwani wa Kata ya Ndugumbi–Magomeni na zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kuchukua fomu ya uteuzi ya kugombea, alijitoa akisema familia yake imemkataza na ili kuokoa jahazi Kambaya alijitolea kuchukua fomu hiyo.

“Waandishi wa habari wenye kumbukumbu vizuri mwaka 2015, Mtulia alikosea kujaza fomu ya uteuzi wa ubunge na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo alimuengua, chama kilifanya jitihada za kukata rufaa na hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimrejesha. Hivi vyote ni viashiria vya Mtulia kujiweka sokoni,” alisema.

Kambaya alisema CUF haikubaliani na hoja ya Mtulia ya kuunga mkono jitihada za kurekebisha uchumi zinazofanywa na Serikali kwa kuwa ilishatolewa tamko na chama chao na haikuwa lazima ili aonekane anaunga mkono aondoke katika chama chake.