Mtulia aanza taratibu za kuomba kura upya Kinondoni

Muktasari:

Maulid Mtulia ametii agizo la CCM lililomtaka kuripoti leo Jumanne ofisi ya CCM mkoa kwa ajili ya kuchukua maelekezo ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (CUF), kisha kuhamia CCM, Maulid Mtulia ametii agizo la chama hicho lililomtaka kuripoti leo Jumanne ofisi ya CCM mkoa kwa ajili ya kuchukua maelekezo ya uchaguzi.

Hatua hiyo imekuja baada ya wiki iliyopita CCM kutangaza kuwarudisha kugombea majimbo yao waliokuwa wabunge Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) na Dk Godwin Molell (Siha-Chadema) ambao wamejiunga na chama hicho tawala.

Mtulia alitangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge Desemba 2 mwaka jana huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishiwa na mtu yeyote na amebaini Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani iliahidi kuyatekeleza.

Wakati Dk Molell alijiuzulu Desemba 14 huku akieleza amefikia uamuzi huo akiwa na akili timamu na hakushinikizwa na mtu yeyote.

Akizungumza na gazeti hili Mtulia amesema tayari ameshatekeleza agizo hilo leo, Jumanne Januari 9, 2017 na ameshakabidhiwa maelekezo hayo ya uchaguzi na viongozi husika wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

“Namshukuru Mungu nimekabidhiwa maelekezo haya ya uchaguzi, ninachosubiri hivi sasa na utaratibu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu uchaguzi wa jimbo la Kinondoni,” amesema Mtulia.

Hata hivyo, Mtulia hakuwa tayari kueleza ni maelekezo ya aina gani badala yake amesisitiza kuwa anaisubiri NEC kutoa utaratibu wa kampeni.

Uchaguzi wa mdogo wa marudio wa  majimbo ya Kinondoni na Siha unatarajiwa kufanyika  Februari 17 baada ya NEC, kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ikieleza majimbo hayo yapo wazi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari wiki iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole alisema baada ya kutafakari na kutathimni kwa kina Kamati Kuu ya CCM imewateua Mtulia na Dk Molell kugombea tena nafasi hizo.