Mtulia awapigia magoti CCM, awaomba radhi kwa kuwashinda 2015

Mgombea ubunge jimbo la Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia

Muktasari:

Mtulia ametoa kauli hiyo leo Januari 21, mwaka 2018 wakati akitambulishwa kwa wanachama wa chama hicho wilaya ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Mgombea ubunge jimbo la Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amewaomba radhi wanachama wa chama hicho tawala kwa ushindi wa kishindo alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 akiwa CUF.

 

Mtulia ametoa kauli hiyo leo Januari 21, mwaka 2018 wakati akitambulishwa kwa wanachama wa chama hicho wilaya ya Kinondoni.

 

Mwaka 2015, Mtulia alishinda ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF,  lakini Desemba 2 mwaka jana alijivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM, hivyo kupoteza sifa ya ubunge. Hata hivyo CCM kilimpitisha kugombea ubunge katika jimbo hilo.

 

Huku akiviponda vyama vya upinzani Mtulia amesema, “Nawaomba msamaha kwa yote niliyowakwaza  wakati wa kampeni na kushinda kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi 2015.”

 

"Mnisamehe mtoto wenu nimerudi nyumbani kwenye chama kubwa. Niliwapa kadi lakini mmeamua kunipa ubunge."

 

Amesema vyama vyote vya upinzani ni sawa na asasi za kiraia, kwamba ni tofauti na ilivyo CCM kwa madai kuwa wapinzani wanasaka pesa na si kusaidia wananchi.

 

Alitaja sababu iliyomfanya kuhama CUF kwamba ni baada ya kuona viongozi wake wakuu hawaelewani, huku akisisitiza kuwa nje ya CCM ni sawa na kujenga ukuta.

 

Mtulia aliambatana na wanachama wa CUF walioamua kujiunga na CCM na kukabidhiwa kadi.