Mugabe asema hakuwahi kufikiria kupinduliwa na Mnangagwa

Muktasari:

"Nasema yalikuwa mapinduzi, baadhi ya watu wamekataa kuyaita mapinduzi," alisema Mugabe akieleza kwa ufupi hatua ya jeshi ambalo lilisababisha Emmerson Mnangagwa kunyakua mamlaka baada ya kujiuzulu kwa Mugabe.


Harare, Zimbabwe. Rais wa zamani Robert Mugabe amefafanua kuondoka kwake ofisini Novemba 2017 kuwa sawa na “mapinduzi” na kwamba "lazima tuzuie" alipozungumza kwa mara ya kwanza katika mahojiano yake kwenye TV Alhamisi.

Mugabe, mwenye umri wa miaka 94, alizungumza polepole lakini kwa uhakika alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) kutoka ofisi kwake Harare, akiwa amevaa suti ya kijivu huku akiwa ameketi mbele ya picha yake mwenyewe na mke wake Grace.

"Nasema yalikuwa mapinduzi – baadhi ya watu wamekataa kuyaita mapinduzi," alisema Mugabe akieleza kwa ufupi hatua ya jeshi ambalo lilisababisha Emmerson Mnangagwa kunyakua mamlaka baada ya kujiuzulu kwa Mugabe.

"Tunapaswa kuifuta aibu hii ambayo tumejiwekea wenyewe, hatukustahili ... Zimbabwe haistahili hali hii."

Katika mahojiano mengine sawa na hayo ya Shirika la ITV News la Uingereza, kiongozi huyo mkongwe alisema hana nia ya kurudi mamlakani. "Sitaki kuwa rais, kwa vyovyote hapana," alisema. "Sasa nina miaka 94."

Mugabe aliyaambia mashirika yote mawili (SABC na ITV News) kwamba hana chuki na mrithi wake Rais Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75, lakini anasema "amelisaliti taifa zima".

Kiongozi huyo aliyeondolewa alisisitiza kwamba hawezi kufanya kazi na Mnangagwa na alidokeza kuwa urais wake ulikuwa "batili" na "kinyume cha katiba".

"Watu wanapaswa kuchaguliwa kuingia serikalini kwa njia sahihi. Nina nia ya kulizungumza hili, na nia ya kusaidia katika mchakato wake - lakini lazima nialikwe," alisema.

Amesema kuwa hakudhani kama angepoteza imani yake kwa Mnangagwa kwani yeye ndiye alimsaidia kuingia serikalini.

“Siamini kama yeye Mnangagwa angeweza kuniondoa madarakani, nimemwingiza serikalini, nilimsaidia alipokuwa jela anataka kunyongwa, sikuwaza kabisa kama siku moja yeye ndiye angekuwa mtu wa kunitoa madarakani,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi mwenye makao yake Johannesburg Afrika Kusini Gideon Chitanga, alisema kuwa kuingilia kati dhidi ya utawala wa Mugabe kulikuwa muhimu "kufanywa wakati uchaguzi ukiwa umewadia".