Muhimbili waja na mbinu ya kupunguza muda wa majibu ya wagonjwa

Muktasari:

  • Akizungumza leo, Jumatatu Februari 19,Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema mfumo huo utatumia vipaza sauti na kompyuta

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeanza kupunguza muda wa kutoa majibu ya vipimo vya magonjwa mbalimbali baada ya kuanza kutumia mfumo wa utambulisho wa sauti.

Akizungumza leo, Jumatatu Februari 19,Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema mfumo huo utatumia vipaza sauti na kompyuta.

Amesema kabla ya mfumo huo, madaktari wamekuwa wakiandika majibu ya wagonjwa kwa mkono na kuwapa makatibu muhtasi wachapishe kwenye kompyuta.

“Madaktari wamekuwa wakiandika majibu ya vipimo kwa mkono, wanawapa makatibu muhtasi ili wachape kwenye kompyuta,” amesema.

Ameongeza, “makatibu muhtasi baada ya kuchapa waliwarudishia madaktari ambao nao walifanya masahihisho ya kilichochapishwa na kurudisha tena kwa makatibu muhtasi.”  

Museru amesema mlolongo huo uliwachukua wagonjwa muda mrefu ili kupata majibu ya magonjwa waliyoyapima.

Amesema mfumo huo mpya, daktari atasoma majibu ya vipimo vya mgonjwa kwa mbele ya vipaza sauti ambavyo vitaingiza sauti kwenye kompyuta.

Amesema vifaa hivyo vitaweka sauti hiyo kwa maandishi na mgonjwa atapata majibu ya vipimo hivyo kwa muda mfupi.

“Mlolongo wa kupata majibu ya vipimo ulikuwa mrefu lakini sasa utapungua baada ya kuanza kutumia teknolojia hii mpya,” amesema.

Amesema majibu yalichukua muda mrefu kwa sababu ya watu wengi wanaohitaji huduma ya vipimo vya maabara na upimaji wa kutumia picha.

Amesema hospitali hiyo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Tiba cha Yale kilichopo Marekani ambayo imekuwa ikitoa mafunzo kwa madaktari wa hospitali ya Muhimbili.

Kuhusu muda utakaotumika, Profesa Museru amesema kwa sasa bado hawajajua watatumia muda gani kutoa majibu kwa kuwa ndiyo unaanza.

“Kwa sasa tunatoa mafunzo kwa madaktari huku tukitumia mfumo huu mpya, baadaye tutaweza kueleza tofauti ya mfumo huu na tulivyokuwa tukitoa huduma hii zamani,”amesema.

Kwa upande wake, Profesa wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Yale, Frank Minja amesema mfumo huo utakuwa wa kwanza kutumiwa na hospitali za Serikali hapa nchini.

“Katika mfumo huu daktari pekee yake atakuwa na uwezo wa kusoma na kutoa majibu ya vipimo kwa wagonjwa bila kumhusisha mtu mwingine na kwa muda mfupi,” amesema.

Amesema kwa sasa wataalam kutoka katika chuo hicho wanatoa mafunzo kwa madaktari wa Muhimbili.

mwisho