Wednesday, October 18, 2017

MultiChoice yasherehekea bethidei ya miaka 20 Tanzania

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Kampuni ya MultiChoice Tanzania inayomiliki king’amuzi cha DStv, imesherehekea miaka 20 tangu ianze kutoa huduma nchini leo Jumatano Oktoba 18,2017.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo, Baraka Shelukindo amesema maadhimisho hayo yatajumuisha maonyesho ya siku mbili yatakayofanyika Mlimani City, Oktoba 19 na 20.  

Amesema DStv ilianza na chaneli tatu za SuperSport, M-Net na Movie Magic na leo inajivunia kuwa na zaidi ya chaneli 100 na redio katika vifurushi vya aina mbalimbali.

Mwanahisa wa Multichoice Tanzania na mwenyekiti wa bodi, Balozi Ami Mpungwe amezungumzia maadhimisho hayo akisema, “Multichoice Tanzania imekuwa bingwa katika kutoa burudani za hadhi ya kimataifa kwa Watanzania. Tulianza huduma zetu katika soko hili wakati ambao biashara ya televisheni ilikuwa changa.”

Amesema kampuni hiyo imegusa maisha ya mamilioni ya Watanzania ikitengeneza ajira 100 moja kwa moja kwenye kampuni,  wafungaji wa DStv wa kujitegemea zaidi ya 1,000 na wauzaji wa moja kwa moja takriban 500.

-->