Mume, mke wafa kwa mafuriko wakitoka kufunga ndoa

Wananchi wa Kata ya Sambasha wilayani Arumeru mkoani Arusha wakiopoa mwili wa mtu aliyefariki kwa kusombwa na maji eneo la Mto Selian jana kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana na kusababisha maafa . Picha na Moses Mashalla

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kwamba tukio la kwanza, lilitokea juzi nne usiku katika eneo la Ngaramtoni, baada ya gari lililokuwa limebeba maharusi waliokuwa wametoka kufunga ndoa na watu wengine, kusombwa na maji katika daraja la Mto Seliani.

Arusha. Watu saba wamefariki dunia kwa kusombwa na mafuriko katika matukio matatu tofauti, wakiwamo mume na mke waliokuwa wametoka kufunga ndoa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kwamba tukio la kwanza, lilitokea juzi nne usiku katika eneo la Ngaramtoni, baada ya gari lililokuwa limebeba maharusi waliokuwa wametoka kufunga ndoa na watu wengine, kusombwa na maji katika daraja la Mto Seliani.

Aliwataja waliofariki kuwa ni maharusi, Munisi Loy (25) na mkewe Nebrise Mungaya (20),  mama ya bwana harusi, Inoti George (40), Ngaisi Moluo na Shengai Saiguran. Alisema dereva wa gari, aina ya Toyota Premio, Yusuf Jacob alinusurika baada ya kushuka kutazama wingi wa maji lakini wakati anarejea kwenye gari alikuta tayari limezolewa.

Katika tukio jingine, mtu mmoja Babu Lobikeki alisomwa na mafuriko alipokuwa akivuka mto katika Kijiji cha Kereiani na tukio la tatu ni la dereva wa bodaboda, Seuri Meseyeki ambaye ni alisombwa na mafuriko katika eneo la  Orelian Ngaramotoni. Matukio hayo mawili pia yalitokea juzi.