VIDEO: MunaLove aweka bayana kilichoibua utata wa baba wa mtoto wake

Muktasari:

Muigizaji huyo wa filamu amesema wakati anaolewa na Peter tayari alikuwa na ujauzito na akaridhia kulea mimba na mtoto.


Msanii wa filamu, Munalove ameweka bayana mkasa wake na Castro Dickson uliosababisha utata wa baba mzazi wa mtoto wake aliyekutwa na mauti mapema mwezi huu.

Mtoto huyo anayeitwa Patrick, alifariki akiwa anatibiwa tatizo la uvimbe kichwani katika hositali ya jijini Nairobi na baada ya taarifa za kifo chake, ilisemekana kuwa msiba ungekuwa Mbezi kwa mama yake, lakini baadaye mtu anayeitwa Peter aliibuka na kusema kuwa yeye ndiye baba wa mtoto huyo na kutaka shughuli hizo zihamie kwake.

Kuibuka kwa Peter ndiko kulikostua wengi waliokuwa wakijua kuwa mtoto huyo ni wa catsro ambaye ni mtangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM.

Lakini jana, Munalove aliita waandishi wa habari nyumbani kwake Mbezi na kueleza jinsi alivyoingia kwenye mahusiano na Castro wakati akiwa bado ana mumewe wa ndoa hadi alipopata ujauzito na jinsi Peter alivyokubaliana na hali yake na kukubali kulea mimba.

"Niliamua kukaa kimya kwa kipindi chote hicho ili kumsitiri mtoto wangu," alisema Munalove alipozungumza na waandishi kwa mara ya kwanza tangu amzike mwanae.

Alisema wakati anaolewa na Peter, tayari alikuwa na ujauzito wa wiki mbili na alimweleza mumewe matarajiwa hali yake.

"Wakati nilipokuwa mjamzito, ndipo nilipokutana na Peter. Nilimweleza kuwa mimi ni mjamzito na Peter alikubali na akasema atakuwa tayari kunilea na ujauzito wangu na akakubali kumlea mtoto," alisema MunaLove.

MunaLove alisema aliishi katika ndoa na Peter kwa takriban miaka miwili na baadaye wakatengana.

"Kila mtu aliendelea na maisha yake; yeye na mwenzake na mimi na wangu," alisema.

Alisema sasa ni miaka mitano tangu watengane na Peter na mumewe na kwamba Peter hakuwahi kumuona mtotom tangu watengane hadi alipofikisha miaka sita.

"Nashashangaa maneno aliyokuwa akiongea kipindi chote cha msiba kama vile hajui lolote lilikuwa likiendelea," alisema MunaLove.

Kuhusu gharama za matibabu ya mtoto, MunaLove alisema yeye ndiye aliyelipia na baada ya kufariki amebaki na madeni makubwa.

"Kama kuna mwanaume aliyenisaidia kumuuguza mtoto, Mungu ndiye anajua," alisema.

"Nilisaidiwa na wasamaria wema akiwemo Mange (Kimambi aliye Marekani) na Zamaradi (Mketema) kuchangaisha. Mercy (Nyagaswa) alisaidia hadi katika kuusafirisha mwili.

"Sijui hao wanaosema kuwa walikuwa wananihudumia mtoto wangu walikuwa wanasema kwa lengo gani hasa. Yote namwachia Mungu kwa kuwa yeye ndiye anayejua ukweli."