Munalove kutumia Sh5 milioni kuondoa tattoo zake

Muktasari:

Hatua hiyo ya kuzifuta inakuja baada ya siku za karibuni kuamua kuokoka kutokana na kupitia majaribu ya mtoto wake kuumwa.

Msanii wa filamu na mjasiriamali Rose Alphonce maarufu 'Munalove' anatarajia kutumia zaidi ya Sh5 milioni kufuta 'tattoo' alizonazo mwilini

Hatua hiyo ya kuzifuta inakuja baada ya siku za karibuni kuamua kuokoka kutokana na kupitia majaribu ya mtoto wake kuumwa.

Akizungumza na MCL Digital, Munalove amesema tangu alipoamua kuokoka ameamua kuachana na mambo mengi ya kidunia na kati ya vitu anavyotaka kuvitoa mwilini mwake ni tattoo.

Amesema mpaka sasa ana michoro mitano kwenye mwili wake ambapo wa shingoni pekee ambao ndio mkubwa kuliko yote na  ameshaulizia bei yake na kuambiwa atapaswa kutoa Sh1.5 milioni kuufuta huo pekee.

"Tayari nimeshaulizia kwa wataalam nchini Thailand ambao wanaweza kunifuta hizi tattoo bila kupata madhara yoyote, wameniambia nitapaswa kuwalipa sio chini ya Sh1.5 milioni, lakini nimewaambia nataka nizitoe zote kwa pamoja ambazo hizi ndogondogo zitakuwa sio chini ya Sh1.2 milioni.

 

"Hivyo ukiangalia zote hapo sio chini ya Sh5 milioni japo bado tupo kwenye mazungumzo ya kuona namna gani wanaweza wakanipunguzia bei,” amesema Munalove.

Akielezea  sababu ya kuamua kuokoka, msanii huyu amesema ni baada ya mtoto wake wa pekee, Patrick kuugua takribani miezi tisa ambapo alifanyiwa upasuaji mara tano na kutokana na mateso aliyoyapata alimshauri kuwa ni vyema akaokoka ili apate kupona.

Kutokana na hilo amesema hata sasa kaachana na kuandaa matamasha ya muziki wa kidunia na kujikita zaidi kuandaa yale ya dini ambapo anatarajia kuyafanya siku moja kuja kuwa makubwa kama ilivyo Fiesta