Monday, September 10, 2018

Muswada uliokwama kwa kukosa akidi kupitishwa leo bungeni

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Muswada wa Sheria Mbalimbali namba 2 wa Mwaka 2018 ambao uliachwa Ijumaa wiki iliyopita kutokana na kukosekana kwa akidi inayohitajika kikanuni, leo utarudishwa kwa ajili ya kupigiwa kura ya uamuzi.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 77(1), akidi kwa kila kikao cha Bunge cha kufanya uamuzi, itakuwa ni nusu ya wabunge wote kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba.

Kushindikana kupitishwa kwa muswada huo kulitokana na Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuomba utaratibu kuhusu akidi ya wabunge kutotimia kufanya uamuzi. Mdee alimweleza Mwenyekiti wa Bunge Najma Giga kuwa kulikuwa na wabunge 67 tu kati ya 393 wakati shughuli hiyo ilipotakiwa kufanyika.

Akizungumza na Mwananchi jana, Giga alisema muswada huo utatolewa uamuzi leo.

“Kesho (leo) utatolewa uamuzi. Ni shughuli ya muda mfupi tu ya kutoa uamuzi,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge, leo wabunge watajadili muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 3 wa mwaka 2018 ambao unajumuisha marekebisho ya Sheria ya Taifa ya Takwimu. Marekebisho hayo yanapendekeza adhabu kwa mtu anayechakata taarifa za takwimu na kuomba kibali katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kabla ya kusambaza takwimu adhabu ambayo inaonekana kuja kuwa mwiba kwa wadau.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema marekebisho hayo yanazuia uchambuzi huru wa takwimu zilizotolewa na taasisi mbalimbali nchini.

“Unakumbuka 2007 nilikamatwa kwa sababu ya kufanya uchambuzi wa taarifa za BoT (Benki Kuu ya Tanzania) kuhusu uchumi? Sijapelekwa mahakamani kwa sababu ya Sheria ya Takwimu haikuwa na kosa hilo. Sasa sheria inafanyiwa marekebisho na nikifanya vile tena, ni jela miaka mitatu. Kifungu kipya cha 24A kinazuia uchambuzi huru wa takwimu zozote zilizotolewa,” alisema Zitto.

Jumanne na Jumatano wabunge watajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa mwaka 2018.

Alhamis, Bunge litapokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo Ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogondogo na mkutano wa 12 utakamilisha shughuli zake Ijumaa Septemba 14.

Bunge limeshapitisha miswada miwili wa Sheria ya kulitangaza jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania wa mwaka 2018.

-->