Muswada wa mafuta wawaka moto Kenya

Spika wa Bunge nchini Kenya, Justin Muturi

Muktasari:

Pendekezo hilo, ikiwa litaridhiwa na Bunge, litawezesha bei ya petroli kushuka kutoka Sh127 hadi Sh118, wakati dizeli itapungua hadi Sh107 kutoka Sh115.

Nairobi, Kenya. Licha ya wabunge kumpinga, Spika wa Bunge nchini Kenya, Justin Muturi amewataka watunga sera hao kuupigia kura Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mafuta.

Spika huyo ameshikilia msimamo huo licha ya wabunge kupiga kelele hivyo kumlazimu kuliahirisha kwa dakika 15 kabla ya kurudi kuendelea na mchakato huo.

Upigaji kura wa mara ya kwanza haukuwa na mafanikio hivyo Spika ameagiza ufanyike tena baada ya muda huo.

Rekodi ya Bunge hilo inaonyesha wabunge 352 wamehudhuria kikao hicho ambao ni zaidi ya 349 wanaotakiwa kupiga kura ya kuupitisha au kuupinga muswada unaowasilishwa bungeni humo.

Mvutano huo umeibuka kwenye muswada wa mabadiliko ya Sheria ya VAT inayotaka kuongeza tozo ya asilimia nane kwenye mafuta yote yanayouzwa nchini humo jambo linalopingwa na wananchi wengi wanaosema itaongeza gharama za maisha.

Spika Muturi ameahirisha Bunge kwa dakika hizo 15 kuwapa nafasi wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kurekebisha mitambo kabla upigaji kura haujaanza upya.