Tuesday, January 16, 2018

Muswada wa umri wa kustaafu kujadiliwa kamati za Bunge

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Vikao vya kamati za Bunge vimeanza huku miongoni mwa miswada itakayojadiliwa ikiwa ni ule utakaoongeza umri wa kustaafu kwa lazima kutoka miaka 60 hadi 65 kwa maprofesa, wahadhiri waandamizi na madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu wa umma.

Marekebisho hayo yapo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba Tano wa Mwaka 2017 ambao utazihusisha sheria tano ikiwamo ya Utumishi wa Umma sura namba 298 ambapo kifungu kipya cha 25A kitaongezwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mohamed Mchengerwa ndio itakayojadili muswada huo ambao utahusisha pia sheria nyingine tano.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju lengo la kuongezwa kwa kifungu hicho ni kuweka kwenye masharti ya umri wa kustaafu kwa watumishi wa umma ambayo hayapo kwenye sheria ya sasa.

“Mapendekezo ya kuongeza kifungu kipya yanalenga kuweka utaratibu mpya wa umri wa kustaafu kwa maprofesa na wahadhiri waandamizi wa vyuo vikuu vya umma na madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu wa hospitali za umma,” alisema.

Alisema mfumo huo mpya unalenga kuongeza umri wa kustaafu wa utumishi wa umma kwa ridhaa kwa maprofesa na wahadhiri waandamizi wa vyuo vikuu vya umma na madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu wa hospitali za umma ili uwe 60 kwa wale wanaostaafu kwa hiari badala ya 55 wa sasa.

Pia, mfumo huo unalenga kuongeza umri wa kustaafu kwa lazima uwe miaka 65 badala ya sasa wa miaka 60 ya sasa.

“Marekebisho haya yanalenga kutekeleza maamuzi ya Serikali yanayolenga kuongeza umri wa kustaafu kwa maprofesa, wahadhiri waandamizi wa madaktari bingwa wa binadamu kutoka vyuo vikuu vya umma na hospitali za umma,” alisema.

Masaju alisema katika maelezo ya muswada huo kuwa kuongeza umri kwa kada hizo kutapunguza gharama kwa Serikali ya kuingia mikataba na wataalamu hao mara wanapostaafu.

Alisema pia uamuzi huo utaongeza muda kwa wataalamu wengine kulitumikia Taifa kwa muda mrefu zaidi na pia kufundisha na kukuza wataalamu wachanga walioko chini.     

-->