Monday, April 16, 2018

Mvua yaleta shida Rukwa, Moro

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi

Mvua zinazoendelea kunyesha zimeharibu miundombinu ya baadhi ya mikoa ikiwamo Rukwa na Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kiando amesema mvua hizo zimeleta madhara yaliyosababisha barabara ya Kioze kutotumika.

Kamanda Kiando amesema Sumbawanga ipo juu, hivyo mvua zinazonyesha maji yake huenda katika ziwa Rukwa na Tanganyika.

“Ziwa Rukwa ndiyo husababisha mafuriko, ambapo madaraja na mashamba yamesombwa ikiwamo la eneo la Kaoze.

“Eneo hili ndiyo abiria wa kutoka Kiteta Majimoto huvuka kwenda maeneo mengi, hivyo sasa wanalazimika wakifika hapo kushuka na kuvuka kwa miguu upande wa pili kupanda gari za kwenda maeneo mbalimbali, ”amesema Kamanda Kiando.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema maeneo ya Mto Kilombero na Kilosa nyumba zilizojengwa pembeni ya mito hiyo zimejaa maji.

Amesema pia nyumba zilizojengwa pembeni ya mto Malinyi pia zimejaa maji.

“Natoa ushauri kwa jamii zilizojenga pembezoni mwa mito na mabonde zichukue tahadhari kwa kuwaondoa wazee, watoto na wagonjwa hususani wakati mvua zinapoendelea kunyesha, badala ya kusubiri hadi hali iwe mbaya.

“Na zile zilizojaa maji hawana haja ya kusubiri waondoke maeneo hayo kwa tahadhari kwa sababu hakuna anayefahamu mvua hizi zitamalizika wakati gani na zitazidi muda gani,” amesema Kamanda Matei.

 

-->