Mvua yaua wanne Z’bar, nyumba zaharibiwa

Muktasari:

Wakazi kutoka katika nyumba 1,021 wamehama baada ya makazi yao kujaa maji

Zanzibar. Mvua zinazoendelea kunyesha visiwani hapa zimesababisha athari mbalimbali ikiwamo vifo vya watoto wanne huku maelfu ya wananchi nyumba zao zikibomoka na kujaa maji.

Taarifa hiyo iliyotolewa juzi na kamati ya kukabiliana na maafa Zanzibar imetoa tahadhari kwa wananchi, hasa wanaoishi mabondeni.

Akizungumzia athari hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame alisema mvua hizo zimesababisha vifo vya watoto wanne, nyumba kujaa maji, baadhi kubomoka kuta na miundombinu kuharibika. Alisema kamati za maafa za wilaya na shehia zimebaini kuwa nyumba zilizoathirika zaidi ni zile zilizojengwa mabondeni.

Makame alisema wamebaini nyumba 2,619 zimeharibiwa kutokana na mvua na upepo mkali na kati ya nyumba hizo, 2,575 zipo Unguja na 44 Pemba.

Alifafanua kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja kuna nyumba 2,097 zilizoathiriwa.

Alibainisha kuwa Wilaya ya Mjini zipo nyumba 654, Magharibi ‘A’ (281) na Wilaya ya Magharibi ‘B’ nyumba 1,162.

Mkoa wa Kaskazini Unguja, nyumba 62 zimeathirika kati ya hizo nyumba 20 zipo Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na 42 zipo Wilaya ya Kaskazini ‘B’.

Kwa upande wa Kisiwa cha Pemba, alisema nyumba 23 zimeathirika katika Mkoa wa Kusini; 15 zipo Wilaya ya Mkoani na nyumba nane Chake Chake.

“Kaskazini Pemba nyumba 21 zimeathiriwa kati ya hizo nyumba 11 zipo Wilaya ya Wete na nyumba tisa Wilaya ya Micheweni,” alisema Makame.

Alifafanua kuwa kati ya nyumba zote zilizoathiriwa na mvua visiwani humo, nyumba 1,021 wakazi wake wamehama kutokana na kujaa maji huku nyumba 460 zikiingiwa na maji na nyingine 1,138 zikiwa zimeangukiwa na miti.

Makame alitaja maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hiyo ni Shehia ya Mtoni Kidatu, Mwera, Kibweni, Sebleni, Kwa wazee, Mtumwajeni, Tomondo, Ziwa maboga, Mwanakwerekwe, Fuoni Jangamizini na Chaani Masingini.

Maeneo mengine ni Chaani Kubwa, Kibeni, Matetema, Kazole, Shehia za Michamvu, Bwejuu, Chwaka, Ukongoroni, Mchangani, Mgwachani, Gando, Kipangani, Uwandani, Ziwani, Kiamboni na Tondooni.