Mvutano wa Kubenea, Komu waipa Chadema sura mpya

Muktasari:

Baada ya mvutano wa maneno kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kauli za wabunge wa Chadema Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) zilizoashiria kama wanataka kukihama chama hicho, Kamati Kuu ya Chama hicho imekutana na kuto adhabu kwa wabunge hao ikiwamo kuvuliwa nyadhifa za uongozi wa chama, kupewa onyo na kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja.


Kwa takribani wiki moja Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepita katika msukosuko mkubwa kufuatia wabunge wake wawili kuzua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Wabunge hao, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) walisambaza sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na kutaka kumhusisha Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na kesi ya matumizi mabaya ya ruzuku ya chama.

Kufuatia tuhuma hiyo Kamati Kuu ya chama hicho iliketi kwa dharura na kuwahojiwa wabunge hao ambapo walikiri kuwa sauti zilizosambaa ni zao na kuomba radhi.

Pamoja na kuomba radhi, wabunge hao ambao ni washirika wa kibiashara katika kampuni ya Halihalisi inayozalisha magazeti ya Mwanahalisi, Mseto na Mawio ambayo yote yamefungiwa, walivuliwa nyadhifa zao ndani ya chama na kubaki na ubunge na kupewa onyo kali ikiwa ni pamoja na kuwekwa nchi ya uangalizi maalumu wa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa utamaduni wa Chadema, watu wengi waliotoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii na mijadala mbalimbali, walitarajia wabunge hao kufukuzwa uanachama, kama ilivyowahi kutokea kwa Zito Kabwe aliyekuwa naibu katibu mkuu, mjumbe wa kamati kuu, Dk Kitila Mkumbo, Mweka hazina, Samson Mwigamba na wengine waliokuwa viongozi wa Bavicha.

Kwa vyovyote, uamuzi huo umeiweka Chadema katika sura mpya ya kuwakumbatia wanachama badala ya ile ya awali ya timuatimua kila linapotokea tatizo ambalo ndani ya chama hicho huliita usaliti.

Kutokana na mazoea hayo, wachambuzi wa masuala ya sayansi ya siasa wanapingana kuhusu adhabu hiyo, baadhi wakisema adhabu hiyo hailingani na kosa walilotenda kwa kuwa linahusu pia jinai.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Michael Francis anasema kamati kuu ilipaswa iende mbele zaidi.

“Kama kweli wamekiri kuhusika na jinai ile, kwa nini waishie kuwavua nafasi za uongozi ndani ya chama na kuwaacha waendelee na ubunge?” alihoji.

Anasema hata kama kigezo cha kuwaachia ubunge kinatokana na kuchaguliwa na wananchi, wangeweza kuwanyang’anya kadi ya chama na kupoteza nafasi hizo.

“Huwezi kukosa adabu kwa chama halafu ukatudanganya wewe ni mwaminifu kwa wananchi ambao wamekuchagua, lazima hilo wangelisimamia kama chama na kuwapa adhabu inayostahili,” anaeleza.

Hoja ya msomi huyo inapingwa na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar Salum Mwalimu akisema kuwa shabaha ya chama hicho si kufukuzana na kwamba wanataka kila Mtanzania awe sehemu ya Chadema.

“Tunataka kila mmoja awe bora katika kutimiza lengo letu. Hawa (wabunge) Kamati kuu iliwahoji na kuwatia hatiani na wakapewa adhabu. Kwa mujibu wa katiba yetu adhabu zipo nyingi si kufukuzwa tu,” anasisitiza na kuongeza kuwa hawapangiwi wakati gani kama chama wachukue adhabu gani.

Mwalimu alienda mbali zaidi akijibu tuhuma za wabunge hao kuwa, suala la kumshambulia ni mwenyekiti wa Chadema si dogo, wanamshughulikia, wanampiga ili aondoke, wanajua sababu ya uimara wake chama kinaendelea kuwa imara.

“Na sisi tunasema Mbowe hajiweki, sisi ndio tunamchagua na tutaendelea kumweka hadi pale tutakapoona tunaweza kufanya mabadiliko ya uongozi. “Hatuwezi kukubali kupigiwa kelele, ataendelea kuwepo ingawa hata yeye hataki ila tunamwambia utakuwa,” anaongeza.

Pamoja na hayo, Dk Michael anaonya kuwa chokochoko za ndani zinaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa Chadema na endapo hawatafanya mabadiliko makubwa ndani ya chama kitawafia mikononi.

Lakini, anasema migogoro katika taasisi yoyote ni chachu katika taasisi hiyo na kwamba wanazuoni wanaamini kwamba taasisi isiyokuwa na migogoro ni mfu.

Aina za migogoro

Kwa umujibu wa Dk Michael, kuna aina mbili za migogoro; mgogoro jenzi na mgogoro bomozi na ili kujua taasisi ipo kwamba katika mgogoro wa aina gani kati ya hiyo, unaangalia chanzo chake.

“Hiki kinachoendelea sasa Chadema unaweza sema ni mgogoro bomoa kwani inahusisha uchumi wa chama. Wanachama wake wanailalamikia taasisi hiyo kwamba haina mustakabali mzuri katika kusimamia masuala ya fedha,” anasisitiza.

“Hata baadhi ya wabunge wameshatoka hadharani kulalamikia suala hilo lakini wapo wanaoishia kukaa kimya na kuchukua uamuzi wa kutokea upande wa pili,” anaongeza Dk Michael.

“Kama hawatakuwa na ‘draft reform’ (mabadiliko makubwa) hali itakuwa mbaya zaidi na kuruhusu chama tawala kuendelea kushika hatamu.”

Msomi huyo anasema kwa sasa CCM imeamua kutumia udhaifu wa Chadema na kujivunia madiwani na wabunge wengi.

Anaongeza kuwa imekuwa bahati kwa wabunge hao wawili kuwa wazi na kusema wanachokilalamikia tofauti na wengine ambao wanaamua kukaa kimya lakini wana dukuduku.

“Hata hawa wanaohama wamechoshwa na mfumo uliopo katika chama chao na kulalamika pembeni, pengine hawawezi kujitokeza kama akina Kubenea; ni lazima chama kichukue hatua,” anaongeza.

Lakini, msomi mwingine, Wakili Peter Mshikilwa anakipongeza chama hicho kwa kumaliza tatizo hilo kwa amani.

“Ukiangalia sasa chama kishapoteza wabunge wake wengi, kuendelea kupoteza wengine kwa kuwafukuza hakuna afya,” anasisitiza.

Mshikilwa anasema chama kimeona umuhimu wa ‘welfare’ (masilahi) ya wananchi ambao wamemchagua mbunge wao ambao ni zaidi ya chama, hivyo endapo wangewafukuza wangewakosesha mwakilishi.

“Wananchi wakikosa mwakilishi haina tija wala afya. Kwenye chama chochote ni pamoja na kukosoana kiitikadi na kimawazo hivyo wale wanaotoka katika mstari ni wajibu wa viongozi kuwarejesha.”

Wakili huyo anaeleza kuwa migogoro katika chama ni mambo ya kawaida na kwa Chadema kuwa na misuguano hakuna ajabu yoyote kwa kuwa bado ni kichanga.

“Migogoro ni hatua ya ukuaji ambayo ni lazima ipitie; tumeshuhudia hata vyama vikongwe kama ANC ya Afrika Kusini walimfukuza mwanachama wake Julis Malema lakini pia walimlazimisha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki kujiuzulu,” anaongeza.

Mshikilwa anasema hata jinsi hatua hizo zilivyochukuliwa zimezingatia misingi ya sheria na kutoa nafasi kwa watuhumiwa kujitetea.

“Demokrasia imefuatwa, kulikuwa na watuhumiwa lakini walipewa nafasi ya kujua makosa yao na kusikilizwa kisha kupata fursa ya kujitetea, ndipo hatua kinidhamu zikachukuliwa,” anasema Mshikilwa.

Maoni ya mitandao

Suala hilo halijavuta tu wasomi, hata kwenye mitandao ya kijamii lilichukua nafasi. Rajabu Sekamba anasema alimwamini sana Kubenea kabla hajaingia kwenye suala hilo, ila kwa sasa imani yake imepungua.

Anasema kitendo cha mbunge huyo kutajwatajwa katika watu wanaotarajiwa kuhama na kutimkia CCM pia kinazidi kumshushia heshima.

Respice Bimbiza anasema; “hongera Chadema kwa kusimamia katiba ya chama na kanuni zake kama wanazingua fukuza.”

Msomaji mwingine, Nixon Jasson anasema, “Nyie tulieni sasa na muwe kitu kimoja kwa ajili ya mustakabali wa hii taasisi kubwa mno msitake kuleteana vurugu zisizokuwa za msingi kama yale ya jamaa wa CUF.

Mega Ismail anasema; “haya ni maono Mungu katuletea na tukiyapuuza yataleta madhara. Asante Mungu kwa kutuonyesha wabaya wetu tunajua wewe watupigania kila siku kumshinda sheteni.

Uamuzi wa Kamati Kuu

Akitangaza uamuzi huo Naibu Katibu Mkuu bara, John Mnyika alisema Kamati kuu iliitishwa na ikafanya kikao chake juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu wa wabunge hao kuwakuta na hatia ya ukiukwaji wa kanuni na maadili ya chama na kuwapa adhabu nne.

Anasema kuwa kwanza Kamati imefikia uamuzi wa kuwapa onyo, pili imewataka waandike barua ya kuomba radhi kwa chama, tatu wabunge hao watawekwa kwenye uangalizi kwa miezi 12.

Kamati hiyo pia iliamua wabunge hao wavuliwe nafasi zao zote za uongozi ndani ya chama na kubaki na ubunge.

Migogoro haijaanza leo

Mara kwa mara Chadema imejikuta ikiingia katika migogoro na kutikisa uhai wa chama hicho mfano ni Machi 10, 2015 chama hicho kilipolazimika kumfukuza uanachama mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Zitto, ambaye hata hivyo alidumu kwenye nafasi ya ubunge kwa takribani mwaka mmoja zaidi kutokana na amri ya mahakama, baada ya hukumu Chadema ilitangaza kumtimua naye akatangaza kujiunga na ACT ambako alipata tena ubunge.

Sintofahamu nyingine ilimuhusisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa baada ya kukutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam kwa mazungumzo.

Kufuatia mazungumzo hayo Lowassa alionekana akimmwagia sifa Rais Magufuli na Serikali yake kwa kazi nzuri inayofanywa.

Kutokana na hilo baadhi ya viongozi wa Chadema na hata wanachama wa kawaida walimshangaa Lowassa kwa uamuzi wake wa kukutana na Magufuli na kummwagia sifa kama alivyofanya wakati wanayo malalamiko kibao dhidi ya serikali.

Miongoni mwa viongozi walioonesha mwitikio wa kutofurahishwa na jambo hilo ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema ambaye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema; “Mh Lowassa umeikosea Tanzania kwa kauli baada ya kutoka Ikulu. Mema yapi umeyaona katika Serikali hii?

Januari 18, 2018 Kamati Kuu ya Chadema iliitishwa kujadili suala la Lowassa kukutana na Rais Magufuli, hasa baada ya viongozi na wanachama wa Chadema kukerwa na kitendo hicho.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho cha kamati kuu, Lowassa alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari akieleza kwamba alishawishiwa arudi CCM.