Mvutano wa wafanyabiashara wa mabasi waibuka Dodoma

Muktasari:

Ni kutokana na baadhi ya kampuni za mabasi kutokuwa na stendi maeneo ya mjini

Dodoma. Mvutano miongoni mwa wafanyabiashara wa mabasi mjini hapa unaotokana na upakiaji holela wa abiria wanaoelekea nje ya mkoa huo umezua hali ya sintofahamu na kuibua usumbufu kwa wasafiri.

Stendi kuu ya mabasi kutoka mikoa mbalimbali iliyopo mkoani hapa ilihamishiwa Nzuguni, umbali wa kilomita tisa kutoka katikati ya mji wa Dodoma, jambo lililotoa nafasi kwa kampuni za mabasi zenye stendi maeneo ya mjini, kupata abiria wengi zaidi.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya kampuni nyingine za mabasi nazo zimeanza kupakia abiria katika stendi bubu, kushinikiza kampuni zenye stendi rasmi maeneo ya mjini nazo kuzuiwa.

Meneja wa kampuni ya mabasi ya Shabiby,  Edward Magawa amesema wana vibali vya kuwaruhusu kupakia na kushusha abiria katika stendi yao, lakini wanashangazwa kuona mabasi yao yakikamatwa.

"Sisi wengine tuna vibali vyote na tumelipia kila kitu, inashangaza tunavyokamatwa jambo ambalo linaleta  usumbufu kwa abiria wetu, yaani ni kero," amesema Magawa.

Amesema mchezo huo unafanywa na washindani wao kibiashara ambao stendi zao hazina sifa na hazijasajiliwa, kwamba sasa wanalazimisha kupakia abiria kwa kulazimisha.

Asha Salehe aliyesafiri na basi la Shabiby kutoka Arusha amesema kitendo cha kulazimishwa wakashushwe Nzuguni na kutumia usafiri mwingine kwenda mjini kinakera, kuwaomba wenye mamlaka kulitazama jambo hilo.

Ofisa habari wa jiji hilo, Ramadhan Juma amesema   kampuni zenye vibali vya kupakia na kushusha abiria mjini ni Shabiby na ABC.

Amesema mabasi mengi yamekuwa yakipakia kwa makosa maeneo ya mjini na hata wanapolalamika si halali kwani Jiji limewapa vibari vya kukatisha tiketi tu.

"Ukiacha Shabiby na ABC hakuna mwingine anaruhusiwa kupakia wala kushusha, hao wanaokamata mabasi ya kampuni hizo wanafanya makosa," amesema.