Mwajiri bora nchini kujulikana Desemba

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka alisema jana kuwa kinyang’anyiro cha kumsaka mshindi huyo kimegawanyika katika hatua mbili.

Dar es Salaam. Mwajiri Bora wa Mwaka 2016, anatarajiwa kujulikana ifikapo Desemba mwaka huu, baada ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kuzindua rasmi tuzo hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka alisema jana kuwa kinyang’anyiro cha kumsaka mshindi huyo kimegawanyika katika hatua mbili.

Dk Mlimuka alisema hatua ya kwanza ni utafiti kwa kampuni zitakazojitokeza kuwania nafasi hiyo chini ya mshauri elekezi.

Alitaja hatua ya pili kuwa ni kutoa tuzo kwa washindi ifikapo Desemba mwaka huu.

Mkurugenzi huyo alisema lengo la tuzo hizo ni kutambua waajiri wenye misingi bora ya usimamizi wa nguvu kazi na rasilimali watu.

Kutokana na kutambua mchango huo, Dk Mlimuka alisema mwaka huu wameongeza tuzo mbili.

Alisema tuzo hizo ni kwa ajili ya kupima ushiriki wa wafanyakazi ili kujua kwa kiasi gani wanahusishwa na kazi wanazofanya, wanajitoa kwa ajili ya waajiri wao na kama wana bidii katika utendaji.

Mkurugenzi huyo alisema tuzo ya pili ni kuangalia umuhimu wa usimamizi wa vipaji na kuviendeleza, lengo likiwa kuwezesha kampuni kuvutia, kutunza, kutoa motisha na kuendeleza mahitaji ya wafanyakazi kwa sasa na baadaye.

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kilianzishwa mwaka 1960 kwa lengo la kuwasilisha na kutetea masilahi yao katika mamlaka mbalimbali, ikiwamo Serikali.