Mwakilishi ahoji Sh2 bil za minara

Muktasari:

  • Said alihoji hayo jana katika Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji, Mohamed Ahmada Salum kuweka wazi kuwa hadi wakati huu bado fedha hizo hazijalipwa.

Mwakilishi wa Chake Chake, Suleiman Sarahan Said amehoji jambo lililosababisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kushindwa kulilipa Shirika la Bandari Zanzibar zaidi ya Sh2.1 bilioni mwaka 2016 zilizotokana na minara ya kuongozea meli za kigeni nchini.

Said alihoji hayo jana katika Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji, Mohamed Ahmada Salum kuweka wazi kuwa hadi wakati huu bado fedha hizo hazijalipwa.

Akihoji suala hilo, Said alisema Shirika la Bandari Zanzibar nalo linahitaji fedha hizo kwa ajili ya kujiendeleza katika shughuli zao mbalimbali.

Akijibu suala hilo Naibu Waziri huyo alisema tayari uongozi wa wizara yake umeshafanya mazungumzo na kamati husika ili kuona jambo hilo linapatiwa ufumbuzi.

Alisema uongozi huo umeshakutana zaidi ya mara moja kujadili suala hilo na hivi karibu wanatarajia kukutana na uongozi wa Wizara ya Mawasiliano ili kulizungumzia suala hilo la kupatiwa ufumbuzi unaofaa kisheria kwa pande zote mbili.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi huyo aliyetaka kujua ni muda gani ambao shirika hilo halijapokea fedha kwa ajili ya malipo ya matumizi ya minara kutoka TPA, alisema shirika hilo lina asilimia yake maalumu ya mapato hayo kila yanapofanyika malipo.

Salum akijibu suala hilo alianza kwa kutoa utaratibu wa fedha zitokanazo na minara hiyo akisema shirika hilo kwa kushirikiana na TPA wanakusanya malipo yote ya matumizi ya minara mikubwa inayotumiwa na meli za kigeni, kisha kila upande hufanya hesabu zake na kulipana kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na mamlaka hizo.