Mwakyembe akumbusha muziki uchaguzi wa 2015

Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe 

Muktasari:

Asema aliponea chupuchupu


Mbeya. Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe ameukubali ‘muziki’ wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwamba aliponea chupuchupu kutokana na kukumbana na  upinzani mkali.

Dk Mwakyembe ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezao aliweka wazi hilo juzi jioni Julai 21, 2018 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho kumnadi mgombea udiwani wa Mwanganyanga- Kyela Mjini, Alex Mwinuka ambao ulifanyika uwanja wa Mtaa wa Mwaikambo huku mgeni rasmi akiwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

“Kyela hatukufanya vizuri sana mwaka 2015, hili naomba ulijue mheshimiwa mgeni rasmi (Dk Tulia)… Aaah!! tulipita chupuchupu hivi… kura za Rais, kura za mbunge hazikuwa nzuri sana. Lakini tulichezewa mchezo usiku na sasa ndiyo tunagundua, zaidi ya theluthi moja ya kura zilipigwa na watu ambao wala hawatoki Kyela,” amesema Mwakyembe na kuongeza:

“Wanatoka Mbozi, Ileje wanatoka Mbeya mjini. Safari hii hata wabebe Bombadia 50 kuleta hapa, kwanza hawapandi Bombadia, tuseme mabasi maana Bombandia wao inawaletea matatizo. Wapanda mabasi hata 50 waje Kyela, CCM tuna ushindi wa kishindo Mwanganyanga, hivyo niwaombe wana CCM Mwanganyanga tuhakikishe Agosti 12 tunampa Mwinuka kura zote.”

Akizundua kampeni hizo, Dk Tulia  aliwataka wananchi wa kata hiyo kutofanya makosa kama waliyoyafanya mwaka 2015  ya kumchagua mtu wa Chadema kwani sasa hivi hawapo kunadi sera za chama bali ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

“Ndugu zangu wana Mwanganyanga hapa hatupo kunadi sera, kwani Serikali iliyopo ni ya CCM ambayo mwaka 2015 mliipigia kura kulingana na sera zake. Hivyo sasa hivi huyu Mwinuka anakwenda kutekeleza Ilani hiyo na si vinginevyo,” amesema Dk Tulia.